Jaribio la mauaji ya Lissu limeacha alama mbaya kabisa katika uso wa dunia ya karne ya 21 na katika nyanja ya ujasusi ulimwenguni, Tanzania imeingia kwenye kikundi cha nchi hatari zaidi kwa binadamu hasa wakosoaji wa serikali na hatari zaidi kwa wapinzani wa kiasiasa sawa na nchi za Rwanda, Burundi, Uganda nk. Tukirejea na matukio ya nyuma na kamata kamata ya wanasiasa.

Mageuzi ya dunia yametokea katika zama nzuri za karne 21, na dunia imewalazimisha watu kugeuka vile itakavyo. Katika uwanda wa kijasusi viongozi wa umma walikuwa wanaondolewa kwa njia nyingi, kama kura, risasi ama sumu. Huo ndio msingi wa wa maisha ya ujasusi wa kidola duniani na nguvu ya ladha ya madaraka. Leo dunia imehama, ipo hapa ilipo na ujasusi wa kidola umehama, njia mpya za kumuondoa kiongozi yeyote madarakani zimepatikana, sio risasi wala sumu tena. Mapinduzi mapya kwa watawala/viongozi ni ya kikatiba ama kisheria. Rejea kuondolewa kwa Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini. Majasusi wanachezea katiba kwa mwavuli wa bunge tu inatosha kumuondoa kiongozi madarakani, mauaji ya risasi leo ni ushamba wa muuaji ambapo kwahakika hajajihakikishia usalama wake.

Sura ya 2, Ukurasa wa 302 wa Kitabu cha Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi kilichoandikwa na Yericko Nyerere, mwandishi anaeleza msingi wa vikosi vya siri vya mauaji na hujuma vilivyo katika nchi ambapo havitambuliwi katika wala kwa sheria za nchi, bali wanaoviongoza wana kinga za kisheria dhidi ya matokeo hasi ya vikosi hivyo. Nikinukuu kutoka kitabuni humo inasomeka hivi,

Shughuli za kijasusi ulimwenguni hasa ujasusi wa kidola unaomilikiwa na kuratibiwa na serikali za ulimwengu, ili shughuli hizo ziwe na mafaa, oparesheni zake zinalindwa na kinga za kikatiba na kisheria. Aghalabu, kinga hiyo humlenga Rais, Waziri Mkuu, Mfalme na/au Malkia ambao ndio washiriki halisi wa taarifu wa oparesheni za kijasusi, na watu hawa, kijasusi na lugha ya Kiingereza huitwa, Spounsor.

Hata hivyo, hapa inategemeana na aina ya mfumo wa taifa husika. Hii inatokana na kwamba, aghalabu, oparesheni za kijasusi hasa zile za siri zaidi hufanywa kinyume na haki za binadamu au kinyume na katiba na sheria za nchi husika. Kwa lugha nyepesi, tuseme, shughuli za oparesheni za kijasusi huenda sambamba na uvunjifu wa sheria za nchi.

Nchini Marekani, Sheria ya Usalama wa Taifa ya Mwaka 1947 (U.S. National Security Act, 1947), Rais amepewa kinga yakutoshitakiwa kufuatia shughuli za oparesheni za kijasusi zinazofanywa na kikosi cha Special Activities Division au kwa kifupisho SAD, kilicho ndani ya CIA kwa manufaa ya taifa la Marekani. Kinga hiyo huitwa, AMRI No 12333 (Executive Order No 12333) ya mwaka 1947 ambapo mwaka 2008, ilifanyiwa marekebisho.

Sheria hii inampa mamlaka Rais wa Marekani kuamuru kufanyika kwa operasheni ya siri pasipo kumuweka Rais kutambuliwa uhusika wake kwenye hilo, iwapo ikitokea siri ya operrsheni hiyo imevuja.

Kwa maneno mengine, Sheria hii inampa uwezo Rais kukana kuhusika kuamuru oparesheni kufanyika au kufahamu chochote juu ya kufanyika kwa oparesheni hiyo ikitokea siri imevuja kuhusu oparesheni hiyo. Hii kitaaluma, na kwa lugha ya Kiingereza hujulikana kama, Plausible Denialbility.

Kutokana kuongezeka kwa changamoto za kimataifa, ambazo nyingine zinatishia usalama au maslahi ya Mrekani lakini Marekani haiwezi kuchukua hatua zozote kutokana kujiepusha na lawama kutoka jamii za kimataifa, ndipo hapo ikaonekana kuna umuhimu wa kuwa na kitengo maalumu kwa ajili ya masuala kama hayo.

Ndipo hapa ambapo, serikali ya Marekani ikaagiza shirika la kijasusi la CIA, kuanzisha kitengo maalumu ndani yake ambacho kitakuwa na maafisa (wanajeshi) ambao wanaweza kutekeleza oparesheni yoyote ya kijeshi kwa kujitegemea pasipo kuhusisha serikali ya Marekani. CIA wakaanzisha idara maalumu ndani yake na kuiita Special Activities Division au kwa kifupisho, SAD, ambayo idara yenyewe ilikuwa na maafisa wa siri ambao hawabebi vitambulisho na majina yao ni siri kubwa hayawezi kupatikana hata kwenye orodha ya maafisa wa CIA.

Lengo kubwa la kuanzishwa kwa idara hii ni kutekeleza oparesheni maalumu za kijeshi au propaganda na ikitokea wakakamatwa au kushitukiwa basi serikali ya Marekani wanawakana kuwa si maafisa wao. Kwa hiyo, kitengo hiki, kilikuwa kinafanya kazi kwa niaba ya serikali ya Marekani lakini kulikuwa hakuna uwezekano wowote wa adui kuunganisha uhusika wa kikosi hiki na serkali ya marekani.

Ndani ya Idara hii ya SAD, kuna vitengo vidogo viwili vikuu. Kitengo cha kwanza, kinaitwa Political Action Group ambacho kazi yake kubwa ni kufanya ushawishi wa kisiasa, oparesheni za kisaikolojia na vita vya kiuchumi. Pia, kutokana na maendeleo ya kiteknolojia, kitengo hiki kimeongezewa jukumu la vita vya kimtandao. Tuchukulie kwa mfano, katika nchi fulani kuna serikali au mwenendo wa serikali unaotishia maslahi ya Marekani basi kitengo hiki kinaingia kwa siri kubwa na kufanya mojawapo ya mambo ambayo nimeyaorodhesha hapo juu.

Moja ya matukio ambayo kitengo hiki kimehusika sana na CIA wamekiri kwenye nyaraka zilizowekwa wazi mwaka 2013, ilikuwa ni kueneza propaganda ambayo ilichangia kupinduliwa kwa Waziri Mkuu wa Iran mwaka 1953 ambapo kisa hiki kinaelezwa kwa kina katika kitabu hiki cha Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi. Pia kitengo hiki kilitumika kuzuia Chama cha Kikomunisti cha Italia kushinda uchaguzi mwaka 1960.

Kitengo hiki kimewahi kufanya oparesheni ya siri iliyoitwa Operation Mockingbird katika taifa la Marekani. Oparesheni hii ilikuwa na lengo la kudhibiti habari zinazoandikwa na Vyombo vya Habari nchini humo. Oparesheni hii imekuja kupingwa vikali siku za karibuni na baraza la seneti kwa kuwa sheria hairuhusi CIA kufanya oparesheni yeyote ndani ya ardhi ya Marekani.

Kitengo cha Pili, kinaitwa Special Operations Group (SAD). Kitengo hiki kinajumuisha wanajeshi wenye ustadi wa hali ya juu kutekeleza malengo ya kivita pasipo kujulikana uhusika wa serikali ya Marekani. Ili kulinda utambulisho wao, wanajeshi wa kikosi hiki maalumu hawavai sare za jeshi wala kubeba vitambulisho. Inaelezwa kuwa hiki ndio kikosi maalumu cha oparesheni za kijeshi chenye usiri mkubwa nchini marekani.

Maafisa wote wanaojiunga katika kitengo hiki maalumu cha SAG wanachaguliwa kutoka katika vikosi vingine vyenye weledi vya jeshi la Marekani, mfano; Army Rangers, Combat Controllers, Delta Force, 24TH STS, US Army Special Forces, Navy SEALs, Force Recon, tukitaja vichache. Wakishachaguliwa, wanapelekwa katika kituo maalumu cha mafunzo ya CIA, kilichopo Virginia, kinachojulikana kama Camp Peary (au maarufu kama The Farm) ambapo miezi 18 ya kwanza wanafundishwa kuhusu intelijensia na ushushushu. Baada ya miezi 18, wanapelekwa kwenye kituo kingine cha CIA, kilichopo California, ambacho kinajulikana kama The Point.

Hapa wanafundishwa mafunzo ya hali ya juu ya kijeshi ambayo hayapatikani kwa kiwango hicho katika vikosi vingine vya Marekani. Mfano, wanafundishwa; mapigano ya mikono ya kiwango cha juu zaidi, kutumia karibia aina zote za silaha na milipuko ya jeshi la Marekani na nchi za kigeni, ufuatiliaji adui, kukabiliana na hali ngumu kwenye mazingira ya kawaida na nyikani, kumkwepa aduia, kuzuia adui na kumtoroka adui. Pamoja na mafunzo hayo, anaongezewa kozi maalumu ya kutambua fiziolojia ya binadamu (Udaktari).

Afisa ambaye anafuzu mafunzo haya kwa muda wa miezi 36 anakabidhiwa katika idara ya SAD ndani ya CIA na anatambulika kama Afisa Mwenye Ujuzi Maalumu. Katika oparesheni zao, maafisa hawa huzitekeleza katika vikundi vya watu wachache sana wasiozidi sita na oparesheni nyingine zinatekelezwa na Afisa mmoja pekee. Katika Ofisi za CIA, zilizopo kitongoji cha Langley jijini Virginia, kuna ukuta wa majina ya Maafisa wa CIA waliotunikiwa tuzo za heshima kutokana na utumishi wao uliotukuka. Majina ya maafisa wengi kwenye ukuta huo ni ya wale waliotumikia kitengo cha SAD ndani ya CIA.

Kwa kuzingatia kwamba kitabu hiki kinalenga kuzungumzia ujasusi na kinga ya kijasusi, hapa itaoneshwa uhusika wa CIA katika mapinduzi ya serikali ya Iran kama mkakati uliotekelezwa kwa kinga halisi ya kisheria. Hivyo basi itatolewa mifano michache ya oparesheni zilizotekelezwa na kitengo hiki cha SAD ndani ya CIA.

Ni idara hii maalumu ya CIA ambayo ilikabidhiwa raia wanne wa Tibet kutoka kwa kaka mkubwa wa kiongozi wa kiroho wa Tibet, Mtukufu Dalai Lama, ambapo idara ya SAD iliwapa mafunzo ya kikomando Watibeti hao wane, halafu wakawarudisha Tibet kutafuta raia wengine 300 ambao SAD iliwapa mafunzo ya kijeshi kwa siri katika Kisiwa cha Saipan. Ilipofika mwezi Oktoba, SAD iliwaongoza wanajeshi hawa mpaka Tibet, kuanzisha vuguvugi la kudai kujitenga na China.

Pia, ni kikosi maalumu hiki cha idara ya SAD ambacho kilimtorosha kwa siri Mtukufu Dalai Lama kwa kupita katikati ya majeshi ya China yaliyokuwa mpakani na kumpeleka India. Mpaka leo haijulikani ni namna gani waliweza kufanya tukio hili.

Ni idara hii ya SAD ndani ya CIA ambayo ilihusika kuwapatia mafunzo ya kijeshi raia wa Cuba waliokuwa wanaishi uhamishoni na kuwaongoza katika jaribio la kumpindua Fidel Castro. Mapigano haya ya kihistoria yalidumu kwa siku tatu na yanajulikana kwa jina maarufu la Bay Of Pigs Invasion.

Jaribio hili la mapinduzi halikuwezekana na ndilo lililochangia kudorara kwa mahusiano kati ya Marekani na Cuba mpaka alipokuja Rais Barak Obama wa Marekani na Raul Castro wa Cuba, wakamaliza uhasama huo, mwaka 2014.

Kwa mujibu wa nyaraka za siri za CIA zilizowekwa wazi mwaka 2004, Amri ya kumpiga risasi Che Guevara ilitoka kwa makomado wa SAD. Jeshi la msituni lililojiita Jeshi la Ukombozi la Bolivia (National Liberation Army of Bolivia) lilianzisha vita dhidi ya serikali ya Bolivia ambayo ilikuwa inaungwa mkono na Marekani. Jeshi hili likuwa na vifaa vya kisasa na liliungwa mkono na mwanamapinduzi Che Guevara. Katika hatua za mwanzo za mapigano jeshi hili la waasi lilionekana kushinda dhidi ya majeshi ya serikali. Ndipo hapo CIA wakatuma makomando wa kitengo cha SAD ambao walienda kutoa mafunzo kwa majeshi ya Bolivia katika Milima ya Camiri.

Na baada ya hapo, wakawaongoza kupigana na waasi na kufanikiwa kuwashinda. Kisha makomando wa SAD wakawaongoza makomando wa jeshi la Bolivia (Bolivia Special Forces) kumkamata Che Guevara ambapo mara tu baada ya kukamatwa, komando wa SAD aliyeitwa Felix Rodriguez akaamuru auwawe.

Hii ni mifano michache kati ya mifano mingi amabayo CIA kwa kutumia kitengo cha SAD wameendesha opesheni maalumu za kijeshi katika nchi nyingi. Ingawa Rais wa Marekani ndiye anayetoa amri ya kufanyika kwa operesheni hizi za kuvamia kijeshi nchi nyingine au kuongoza mapinduzi ya serikali halali duniani kote lakini analindwa na sheria ya Marekani ambayo inampa Rais uwezo wa kukana uhusika wa Rais wa Marekani kutoa amri au kufahamu kinachofanywa na kitengo hiki (Plausible Deniability). Sheria hii ilitungwa mwaka 1947, inayojulikana kama National Security Act. Pia, Sheria hii ilitiliwa mkazo na Tamko la Rais Na. 12333 (Executive Order 12333) lenye kichwa cha habari, National Intelligence Activities.

Aidha, huko Israel, Waziri Mkuu anayo kinga kama hiyo, inayompa nguvu ya kuamuru kitengo kidogo cha Mossad kiitwacho Kidon kuendesha oparesheni yoyote ulimwenguni kwa manufaa ya Israel.

Rais wa Tanzania, pia anayo kinga inayolindwa kikatiba ambayo inampa nguvu ya kuamuru oparesheni yoyote ya siri ya kijasusi na katika utekelezaji ikitokea kosa lolote, yeye hashitakiwi popote na yeyote. Ibara ya 46 (1), (2) na (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 inatoa nguvu ya mamlaka ya kijasusi kwa Rais na kumhakikishia kinga thabiti. Pia, sheria ya 1984 Na. 15, ib. 9 na Sheria ya 1992 zinampa Rais kinga, kwa kosa lolote atakalotenda akiwa madarakani.

Tatizo kubwa linalojitokeza katika kinga hizo ni kwamba viongozi wengi wa mataifa wenye uvunjifu wa kimaadili ikiwemo Afrika, hawazitumii kinga hizo kwa manufaa ya mataifa yao bali manufaa binafsi na vibaraka wao wanaowazunguka. Mifano hai ni mingi, lakini hebu tuangazie michache,

Rais wa Rwanda Paul Kagame alipoingia madarakani aliunda kikosi chake cha mauaji ya wapinzani wa Kagame wakipewa jina la maadui wa taifa, kikosi hicho kipo mpaka sasa, kinaitwa Escadron dela Morta ambapo mfanyabiashara maarufu nchini humo Apollo Gafaranga alikuwa mmoja wa wana kikundi hicho. Lengo kuu la kikundi hiki, limekitwa juu ya kuwatafuta wale wote walio kinyume na utawala wa Rwanda na kuwamaliza (yaani kuwafuta kwenye nyuso za ulimwengu). Rejea mauaji ya Patrick Karegeya yanayopatika katika kitabu cha Ujasusi wa Kidola na Kiuchumi Sura ya 2, Uk wa 217.

Pia mashirika ya kijasusi hasa ya kiserikali yana uamuzi wa siri ambao huitwa sheria ya siri ya uamuzi (secrete code) yakumuondoa kiongozi (rais,waziri mkuu) wanchi anapokwenda kinyume na sera na matakwa ya mashirika hayo hasa akiashiria kuleta uvunjifu wa amani ya nchi. 

Uamuzi huu hautambuliwi kwa sheria ya wazi bali ni kama haupo lakini hufanya kazi kwa siri kubwa. Rejea nadharia ya John McCone katika ripoti ya CIA na FBI juu ya mauaji ya John F. Kennedy (Approved for release: 2014/00/29 C06185413).

Tanzania ipo katika vita vya kiuchumi kwa mjibu wa Rais wa Nchi, japo hajatuambia tunapambana na nani katika vita hivi, kwakuwa wanaoitwa wezi wetu waliletwa na anayewaita wezi, lakini kwa asili ya uchumi wa Afrika Mashariki, mtani wetu wa jadi wa uchumi wetu ni Kenya, ambaye kwa sasa ametupita, yeye sasa anapigana vita vya kiuchumi na Afrika Kusini, Misri na Nigeria, huku Rwanda ameibuka kuwa adui yetu mpya katika vita hii, japo ndio msingi wa dunia mpya.

Tukio la Lissu ni la kiuhalifu, sio la kiserikali, halikai meza ya kiserikali na wala halina ladha ya kiserikali ama kitaasisi, Hoja hapa inaweza kuwa, je, serikali za mataifa zinaweza kuwa na makundi ya kihalifu,ujambazi,ugaidi? Jibu ni NDIO, Rejea mtiririko wa makala yangu hapo juu. Na hapa ndipo msingi wa madai ya Chadema kwamba wanahitaji wachunguzi huru wa kimataifa yanapopata nguvu.

Nani alitaka kumuua Lissu na kwa faida ya nani? Kesi hii ni lazima tuanzie nje ya mipaka yetu kurejea ndani ya nchi, adui anaweza kuwa wa ndani au wa nje, anaweza kuwa na malengo ya kisiasa au ya kiuchumi, anaweza kuwa na malengo kiserikali au ya kikanda.

Ni wakati wakutafakari pamoja kama taifa huku tukimsaidia Rais kupambana na uhalifu huu unaochafua serikali ya Rais wetu mpendwa.

Na Yericko Nyerere