​Muda mfupi baada ya kula kiapo, Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangalla, ametoa onyo kali kwa majangili nchini na kuwataka kuacha mara moja vitendo hivyo.

Dkt. Kigwangalla ametoa onyo hilo leo(Jana) Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuapishwa mawaziri na naibu mawaziri. “Majangili waanze kukimbia wenyewe pale wanapowaona wanyama kwani tutawashughulikia ipasavyo na kuhakikisha tunakomesha vitendo hivi viovu katika nchi yetu,” alisema Dkt. Kigwangalla.

Kuhusu utalii, Dkt. Kigwangalla amesema kuwa watalii wamekuwa wakiongezeka lakini si kwa kiwango cha kuridhisha hivyo Serikali itafanya juhudi za makusudi kutangaza vivutio vya utalii kwa njia za kisasa ndani na nje ya nchi. Amesema kuwa ubunifu katika kujitangaza itabidi utumike ili kuhakikisha Tanzania inavutia watalii wengi kutoka nje hususan soko jipya la China na nchi nyingine ikiwemo Marekani na nchi za Ulaya.


Kwa kufanya hivyo pato la Taifa kutokana na utalii litaongezeka kuliko ilivyo sasa, alisema Kigwangalla.Aidha, Waziri huyo wa Maliasili na Utalii amesema atashirikiana na wizara nyingine kukomesha migogoro ya wakulima na wafugaji ili lipatikane suluhisho la kudumu.