Richard Kayombo.
Makusanyo ya kodi kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 (Julia, Agosti na Septemba) yamefikia Sh3.65 trilioni ambayo ni ongezeko la asilimia 1.2 ukilinganisha na makusanyo ya kipindi hicho kwa mwaka uliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo amesema makusanyo hayo ni hatua nzuri kuelekea lengo la mwaka ambalo ni Sh17 trilioni.
Ametoa mchanganuo wa makusanyo hayo kwa kila mwezi ambao umeonyesha kuwa wamekusanya zaidi ya Sh1 trilioni.
“Julai tulikusanya Sh1.1 trilioni, Agosti Sh1.2 trilioni na Septemba Sh1.3 trilioni. Watu wamekuwa wakitaka makusanyo hayo yawe yanasomwa kila mwezi lakini tukitoa kila robo ya mwaka tunaonyesha kiasi kwa kila mwezi,” amesema Kayombo.
Ukizidisha makusanyo hayo mara nne ambayo ni tafsiri ya mwaka mzima jumla inakuwa Sh14.6 trilioni lakini Kayombo anasema makusanyo ya robo moja hayawezi kutoa picha ya jumla kwasababu misimu ya biashara inatofautina hivyo ana matumaini lengo litafikiwa.
 
Amevitaja vyanzo vikuu vya mapatio kuwa ni viwanda, ajira na uingizaji wa bidhaa lakini amesema vyanzo hivyo hutoa kodi zaidi kulingana na wakati.
 
Kadhalika Kayombo amewakumbusha wamiliki wa majengo nchi kulipa kodi zao mapema badala ya kusubiri mwishoni mwa mwaka na kusababisha misongamano na usumbufu usio wa lazima.
 
Pia wamewataka wenye michezo ya bahati nasibu wametakiwa kulipa kodi zao kama sheria inavyoelekeza. “Anayepaswa kulipa kodi kwa wiki alipe na anayepaswa kulipa kwa mwezi au mwaka naye afanye hivyo.”
 
Kayombo amewataka wananchi kutumia na kuziamini takwimu zinazotolewa na mamlaka hiyo kwani takwimu zote nyingine kuhusiana na mapato ambazo hazijatolewa na TRA sio za kuaminika.