Idadi ya wakazi Dar Es Laam niliona Kinondoni walikuwa 1,775,049, Ilala walikuwa 1,220,611 na Temeke walikuwa wananchi 1,368,881 huku jumla ya wakazi Dar Es Laam walikuwa 4,364,541. Hiyo ni Dar Es Laam tu na wilaya zake sitaki kuzungumzia idadi ya Watanzania, lakini wakati nasoma idadi ya wananchi wa Iceland ambao jana wamefudhu kwenda kukipiga kombe la dunia mwakani nilitikisa kichwa.

 

Nilitikisa kichwa nikaamini kweli ukubwa wa pua sio wingi wa kamasi, taifa la Iceland kutoka bara la Ulaya kuna idadi ya wananchi 330,000 tu yaani idadi ya taifa zima la Iceland ukizidisha mara 10 na zaidi ndio unapata idadi ya wananchi wa Dar Es Laam. Mara ya mwisho kwa timu ya taifa yenye wananchi wachache kushiriki kombe la dunia ilikuwa mwaka 2006 ambapo Trinidad & Tobago walienda kombe la dunia huku wakiwa na jumla ya wananchi milioni 1.3.

 

Katika kundi lao hawakuwa wanapewa nafasi sana na wengi waliamini majina na mpira unaopigwa na Wacrotia utawapeleka kombe la dunia lakini haikuwa hivyo, Iceland wametangulia tena wakiongoza kundi lao. Hadithi ya kuvutia zaidi ambayo wakati mwingine inasikitisha ni kwamba wakati tunapiga porojo kupanda viwango vya FIFA, Iceland walikuwa nafasi ya 131 miaka minne iliyopita baadae wakaja na mikakati kushiriki Euro lakini sasa habari imebadilika wanaelekea Urusi.

 

Baada ya ushindi wa jana dhidi ya Kosovo kocha wa timu ya Kosovo alisema timu ya taifa ya Iceland iwe hamasa kwa timu ndogo ambazo hazina matumaini ya kufanya mamubwa na waitumie Iceland kuamini lolote linawezekana.