Ikiwa zimesalia siku mbili kuadhimisha Siku ya Mwalimu Nyerere, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni imefanya usafi wa mazingira katika nyumba ya Baba wa Taifa iliyopo Mikocheni jijini hapa.Kamati hiyo imeongozwa na mkuu wa wilaya hiyo, Ally Hapi ikihusisha askari 417 kutoka Jeshi la Wananchi(JWTZ), Magereza, Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) pamoja na Jeshi la Polisi.Akizungumza mara baada ya kufanya usafi huo leo Alhamisi, Hapi amesema katika kumuenzi muasisi wa Taifa hili usafi wa mazingira ni moja ya njia ya kuunga mkono jitihada zake kwa vitendo.”Hatuna kitu cha kumlipa kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa Taifa hili lakini kwa hiki tulichokifanya ni sehemu ya kumuenzi kwa vitendo,” amesemaAmesema kazi hiyo itakuwa endelevu ikihusisha na maeneo mengine kwenye wilaya hiyo kwa lengo la kuhamasisha wananchi kulinda mazingira.”Kazi hii ni endelevu na itafanyika kila mwezi tukianzia hapa nyumbani na maeneo mengine ikiwamo fukwe za bahari na yale yenye vichaka,” amesema Hapi.
Mjukuu wa Mwalimu Nyerere, Sophia Nyerere ameishukuru kamati hiyo na kwamba wamefarijika kushirikiana katika kuboresha mazingira.