George Opong Weah.
MWANASOKA wa zamani George Opong Weah wa Chama cha Congress for Democratic Change, (CDC)anaongoza, katika matokeo ya awali ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa Liberia uliofanyika hivi karibuni.
Takwimu kutoka tume ya uchaguzi (NEC) zinaonyesha Weah yupo mbele kwenye majimbo 11 kati ya majimbo 15 japo kura zote hazijahesabiwa. Mgombea anayefuatia ni Makamu wa Rais wa sasa, Joseph Boakai, ambaye anaongoza katika jimbo moja na mengine yanayosalia ameshika nafasi ya pili.
Akitangaza matokeo hayo ya awali, Mwenyekiti wa NEC, Jerome Korkoya, amesema kura zilizopigwa katika vituo 1,232 (sawa na asilimia 22.9) zilikuwa zimehesabiwa kati ya vituo 5,390. Weah ameshinda wilaya ya Bomi kwa kura 3,763, wakati Boakai alipata kura 2807.
Huko Grand Bassa, Weah alipata kura 28,233, na Boakai akipata 24,360. Matokeo ya jumla ya mshindi wa urais yatatangazwa Oktoba 25, mwaka huu ambapo mshindi katika kinyang’anyiro hicho analazimika kujipatia asilimia 50 ya kura zote ili aweze kutangazwa mshindi, na kama hakuna mgombea atakayefikisha kiwango hicho, uchaguzi wa marudio unapaswa kuwa mwezi Novemba.
Atakayetangazwa mshindi anachukua nafasi ya mwanamke wa kwanza Afrika kuwa rais, Bi. Ellen Johnson Sirleaf, anayemaliza muda wake kwa mujibu wa katiba ya taifa hilo na ambaye pia aliwahi kuwa Mshindi wa Tuzo ya Nobel.