Benki ya watu  Zanzibar (PBZ) imetoa msaada wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 50 kwa Mkuu mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ikiwa ni kuunga mkono jitihada zake za ujenzi wa ofisi za walimu 402 katika mkoa huo.
Wakati akikabidhi hundi ya fedha hizo Mkurugenzi mtendaji wa Benki hiyo Juma Ameir Hafidhi amesema mbali na kuunga mkono jitihada za Mh Makonda wamelazimika kufanya hivo kwawakuwa asilimia 53 ya faida ya benki hiyo inatoka kwenye matawi yaliyopo Jijini Dar es salaam ambapo amemuhakikishia wataendelea kuchangia maendeleo ya mkoa huo.
Mara baada ya kukabidhiwa fedha hizo akiwa katika makao makuu ya PBZ Visiwani Zanzibar Mh: Mkonda ameishukuru benki hiyo na kuwaeleza kuwa fedha hizo walizotoa zina thamani ya mifuko ya saruji elfu 50, sawa na zaidi ya Matofali laki moja yatakayo saidia ujenzi wa Ofisi za walimu 402.
RC Makonda amemueleza Mkurugenzi  huyo kuwa chachu ya ujenzi ilitokana na changamoto ya shule kubainika hazina Ofisi za walimu nakulazimika walimu kufanyia shughuli zao kwenye madarasa, chini ya miti na wakati mwingine kwenda kumaliza haja zao kwenye Baa na nyumba zilizo jirani na shule na kwamba anaamini kukamilika kwake kutaondoa kama sio kumaliza changamoto hiyo.
Aidha amesema Benki ya PBZ imeungana na Benki ya CRDB ambayo tayari imeweka Dawati maalumu kwenye kila Tawi la Bank hiyo kwaajili ya wananchi wanaotaka kuchangia Ujenzi wa Ofisi za Walimu ambapo Mwananchi anaweza kuchangia kiasi chochote cha Fedha ambapo wengine wataweza kuchangia kwa SimBank.
Amesema kuwa kazi ya ujenzi wa Ofisi za kisasa za Walimu inafanyika Usiku na Mchana chini ya Vijana wenye morali ya kufanya kazi kutoka JKT, Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi ambao Wamemuunga Mkono RC Makonda.
Makonda amewapongeza wadau waliomuunga mkono na wanaoendelea kumuunga mkono katika kufanikisha kampeni hiyo ambapo amewaomba Wananchi kumuunga mkono.
Amesema kuwa hadi sasa amefanikiwa kupata wadau walioahidi kufunga miundombinu ya vifaa vyote vya umeme ikiwemo Taa, Feni ambapo wengine wametoa Mabati 10,000 huku wengine wamejitolea kuweka Vifaa vyote vya Vyoo.