Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amefanya ziara ya siku moja katika maeneo mbalimbali kwaajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu visiwani Zanzibar katika mkoa wa Mjini wa Magharibi.
 Akiongozwa na mwenyeji wake ambaye ndiye Mkuu wa mkoa huo Ayoub Mahamoud ziara hiyo imeanzia katika Pango la Tumekuja lilijengwa enzi za utawala wa Sultan Said Said Barghash kwaajili ya kusafirishia watumwa.
Alitembelea makumbusho ya jengo ambalo lililkuwa likitumika kuuzia watumwa enzi za Ukoloni ambalo lilifungwa rasmi mwaka 1873 na sasa eneo hilo linatumika kama kanisa “Kanisa la Mkunazini” mbali na kutumika kama sehemu ya Historia visiwani humo.
Kabla ya kuelekea mtoni marine inakojengwa hoteli kubwa Afrika mashariki ambayo iko mjini na yenye uwezo wa kupokea wageni wenye meli zao 12,  alitembezwa katika eneo darajani unapofanyika ukarabati wa Jumba la treni ambalo limo kwenye Orodha ya urithi wa dunia.
Pia alitembezwa katika eneo la Nyamanzi unakofanyika ujenzi ya makazi ya kisasa ya nyumba za mbao ambazo zinajengwa hadi kukamilika kwa muda wa siku tisa.
 
Baada ya hapo alitembelea kiwanda cha sukari cha Zanzibar Sugar Factory (ZSF) kilichopo Mahonda Wilaya ya Kaskazini B Unguja chenye uwezo wa kuzalisha tani 80 ya sukari kwa siku.
Ziara hiyo ilihitimishiwa kwenye shamba la Viungo la ‘Spice Farm’ la Kizimbani lenye viungo vya chakula na mboga mboga ikiwemo Tangawizi, Binzari, Pilipili Manga, Karafuu, mdalasini, Hiliki, mchaichai na kadhalika.
Mara baada ya ziara hiyo Mh: Makonda ameeleza sababu zilizomfanya afanye ziara hiyo licha ya kujifunza masula kadhaa ni pamoja na kujadili namna gani watabadilishana taarifa za kiusalama, ukomeshwaji wa biashara ya ngono, dawa za kulevya na kwa upande wake mwenyeji wa mkoa huo Mkuu wa mkoa RC Ayoub ameeleza kuwa baada ya Ziara hiyo wataanza rasmi kurasimisha mahusiano hayo.