Moja ya magonjwa hatari sana ambayo yanaweza kumpata mtu yoyote ni ugonjwa wa shambulizi la moyo. Huu ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha vifo vya wanaume na wanawake.Kwa kawaida, ugonjwa huu hutokea pale ambapo sehemu ya nyama ya moyo inapoharibika au kufa kutokana na kukosa damu ya kutosha.

Je tatizo hili husababishwa na nini?
Husababishwa na kuziba kwa mishipa ya damu inayosambaza damu katika moyo (coronary artery blockage) kutokana na mafuta mabaya mwilini (atherosclerotic plaque).

Watu gani wapo katika hatari ya tatizo hili?
Watu walio katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa huu ni pamoja na

 

Wenye umri mkubwa miaka 45 kwa wanaume na 55 kwa wanawake
Wavutaji wa sigara
Watu wenye mafuta ya lijamu katika damu au wale wenye mafuta mabaya aina ya triglycerides na low density lipoprotein kwa kiwango kikubwa katika damu zao
Wenye kisukari
Wenye matatizo ya shinikizo la damu
Walio na unene kupita kiasi (obesity)
Wenye matatizo sugu ya kushindwa kufanya kazi kwa figo zao (chronic renal failure)
Moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure)
Wanywaji wa pombe kupindukia
Watumiaji wa madawa ya kulevya hasa cocaine na methamphetamine
Watu wenye msongo wa mawazo (Chronic high stress levels)
Upungufu wa vitamin B2, B6, B12 na folic acid

Dalili za shambulizi la moyo

Maumivu makali ya ghafla kifuani ambayo husambaa kwenye taya, shingo, bega na mkono wa kushoto
Kupumua kwa shida
Kutoka jasho kwa wingi sana (diaphoresis)
Kuhisi mapigo ya moyo yanapiga haraka (palpitations)
Kichefuchefu
Kutapika
Kuchoka haraka sana
Kupoteza fahamu

Shambulizi la moyo limehusishwa na nini?
Tafiti mbalimbali zimeusisha mambo yafuatayo na shambulizi la moyo

Msongo wa mawazo
Maambukizi hasa vichomi vinavyosababishwa na vimelea vya chlamydophila pneumonia.
Hutokea zaidi asubuhi hasa saa tatu (saa 3 asubuhi)

 

Vipimo na uchunguzi

ECG – Kipimo hiki huonyesha ni sehemu gani ya moyo iliyoathirika
Coronary angiography – Kinasaidia kwa kuangalia wapi ambapo mishipa ya damu imekuwa membamba sana kupita kiasi (narrowing of vessels) au imeziba.
Cardiac markers levels
X-ray ya kifua (chest X-ray)
MPI (Myocardial Perfusion Imaging) – Kipimo hiki hufanywa kwa kutumia mashine maalum ya PET Scan ambapo kinauwezo wa kugundua tatizo la shambulizi la moyo, huchunguza kikamilifu maumivu ya kifua, huangalia mwelekeo wa tiba ya kuzuia damu kuganda, hutoa mwelekeo wa ugonjwa wa shambulizi la moyo kama ni mzuri au mbaya, hutathmini ubora wa tiba ya shambulizi la moyo kabla na baada ya mgonjwa kupata tiba, huweza kutambua hata shambulizi la moyo ambalo si rahisi kugundulika kwa kutumia vipimo vyengine na pia hutathmini ukubwa wa tatizo la shambulizi la moyo. Hata hivyo kwa sasa kipimo hiki hakipatikani nchini kwetu.

Ili kuweza kutambua uwepo wa tatizo hili, mwaka 1979, shirika la Afya Duniani (WHO) liliweka vigezo vya kutambua shambulizi la moyo. Vigezo hivyo ni

 

Historia ya kuwa na maumivu ya kifua zaidi ya dakika 20
Mabadiliko katika kipimo cha ECG, na
Kupanda na kushuka kwa kipimo kiitwacho kitaalamu cardiac biomarkers hasa creatine kinase – MB na troponin

Matibabu
Shambulio la moyo ni tatizo linalohitaji matibabu ya dharua. Lisipotibiwa kwa haraka husababisha kifo katika muda mfupi sana tangu mgonjwa apatwe na tatizo. Matibabu ya tatizo hili hujumuisha

Kumpa mgonjwa hewa ya oksijeni

Mgonjwa hupewa vidonge vya Aspirini ndogo kuzuia damu kuganda (thrombolytic) kwa ajili ya kuyeyusha damu iliyaganda na hivyo kuzibua mirija midogo ya damu katika moyo iliyozibwa na kuganda huku kwa damu.
Vile vile mgonjwa hupewa dawa za kuweka chini ya ulimi kiitwacho nitrogylycerin (glyceryl trinitrate) ambazo husaidia kutanua mishipa ya damu (vasodilation)
Dawa ya kutuliza maumivu kwa mfano morphine
Dawa ya kuyeyusha mafuta katika mishipa ya damu kama vile clopidogrel
Kuzibua mishipa ya damu inayosambaza damu katika moyo kwa kutumia – Percutaneous coronary intervention (PCI)
Upasuaji (CABG)

Njia za kuzuia shambulizi la moyo

Kuacha kuvuta sigara
Kufanya mazoezi ya mara kwa mara
Kupunguza unywaji wa pombe
Kubadilisha aina ya mlo. Kupunguza mafuta katika mlo na chumvi.
Kutumia mafuta ya samaki (omega-3 fatty acids)
Kuna utafiti unaosema kuwa uchangiaji damu hupunguza hatari ya magonjwa ya moyo hasa kwa wanaume.

Madhara ya shambulizi la moyo

Moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure)
Matatizo katika mfumo wa mapigo ya moyo (Atrial fibrillation) ambayo hatimaye hupelekea kifo
Shambulizi la moyo kurudia mara ya pili
Kifo cha ghafla (sudden death)