Muigizaji nguli Bongo Movie, Jacob Steven ‘JB’.

AMITABH Bhachchan ni muigizaji maarufu duniani aliyejipatia jina kupitia Tasnia ya Filamu India inayojulikana kwa jina la Bollywood. Kwa wapenzi wa muvi za Kihindi watakuwa wanafahamu habari yake kupitia muvi nyingi zikiwemo Shahenshah, Sholay, Akayla, Don, Mahaan na Yaari Meri.

 

Kwa sasa muigizaji huyu ambaye pia ni muandaji wa muvi, mwanamuziki na mtangazaji ana umri wa miaka 75.

 

Lakini bado anakomaa kwenye soko la filamu na muvi zake za mwisho kuachia ni The Ghazi Attack (2017), Begum Jaan (2017) na Saakar 3 (2017) huku akitegemea kuachia Padman, Thugs of Hindostan na 102 Not Out mwaka unaofuata.

 

Hata hivyo, mbali na kuwa muigizaji, kufanya muziki, kuandaa muvi, kuingiza sauti kwenye matangazo mbalimbali na kushiriki kwenye shughuli nyingi za kijamii, Amitabh amewekeza kwenye makampuni mengi yakiwemo Just Dial, Stampede Capital, Meridian Tech na Ziddu. com. Huyo ndiye Amitabh, mtu ‘busy’ na mwenye historia ndefu Bollwood kama ilivyo kwa muigizaji nguli Bongo Movie, Jacob Steven ‘JB’.

 

JB anaendana na Amitabh si kwa maana ya umri, pengine umri wake unaweza usiachane mbali na waigizaji kama Idris Elba na Leonardo Dicaprio, lakini wanaendana na Mhindi huyo kimafanikio hasa kwa kila mmoja wao kuitendea haki tasnia yake.

 

Katika makala haya, JB anafunguka mambo mengi kuhusu kazi zake, nini amefanya kwenye tasnia, uamuzi wa kupiga chini kuigiza na mambo mengine mengi, shuka naye.

Amani: JB, hivi karibuni umewahi kusema kwamba unataka kupiga chini kuonekana kwenye muvi, kwa nini umefikia uamuzi huo?

JB: Naomba kwanza niweke sawa hili jambo maana nimeona limepokelewa kwa mtazamo tofauti. Ipo hivi, ni kweli nategemea kupumzika kuigiza kwenye muvi lakini si kuacha kuigiza. Nitaendelea kuigiza na kuonekana kwenye tamthiliya lakini kwenye muvi sitaonekana ingawa ujuzi wangu nitaendelea kuutoa huko maana sitoacha kuandaa muvi na kuongoza!

 

Amani: Unategemea kuacha au umekwisha acha?

JB: Nategemea kuacha kwa sababu bado sijaacha. Lakini muvi yangu ya mwezi ujao (Novemba), ndiyo itakuwa ya mwisho. Na ili kuwaaga mashabiki wangu nitaizindua kwa kufanya ‘movie premiere!’

 

Amani: Ni kwa nini umefikia uamuzi huo wakati bado tasnia ya muvi inakuhitaji?

 

JB: Ni kweli tasnia bado inanihitaji lakini hata si kwamba ninaitupa. ‘Taste’ zangu zitaendelea kuwepo na kama unakumbuka kuna baadhi ya muvi nimefanya nikiwa nyuma ya kamera na zimefanya vizuri zikiwemo Bado Natafuta aliyocheza Gabo na Chausiku ya Shamsa Ford. Kuhusu kwa nini nimefikia uamuzi huo, kiukweli nina mambo mengi mno ya kufanya, kwa hiyo nimeona ni bora nizame kwenye tamthiliya na muvi niwaachie watu wengine.

 

Amani: Ni mambo gani hayo uliyonayo?

 

JB: Tamthiliya zinanihitaji, makampuni ninayofanya nayo matangazo kila mara yananihitaji kwenye ziara, nahitajika kuandaa muvi, kampuni yangu ya Jerusalemu inanihitaji, bado Kampuni ya Barazani inanihitaji maana nina hisa lakini pia ni bosi kwenye kitengo cha masoko. Unaweza kuona ni kwa namna gani nakuwa ‘busy’.

 

Amani: Unapozungumzia kubanwa na makampuni unayofanya nayo kazi ni yapi hayo na kivipi, hizo ziara
zinakuwa zinachukua muda gani?

 

JB: Nafanya kazi na makampuni mengi sana. Baadhi yake ni Kiboko na hawa wananitaka kwenye ziara karibia mikoa yote Tanzania, Kampuni ya Datam inayojihusisha na viwanja pamoja na Oxfam.

 

Amani: Mpaka sasa kwenye muvi umefanikiwa kuvuna tuzo ngapi?

 

JB: Tuzo nyingi tu. Mwaka 2008 nilipata Tuzo ya Muigizaji Bora kutoka Vinara Awards, 2011 nilipewa tuzo kama hiyo kutoka ZIFF (Zanzibar International Film Festival) kupitia muvi ya Simu ya Bachelor. Mwaka 2013, tuzo ya filamu bora kutoka Steps kupitia Muvi ya Shikamoo Mzee na Kipindi cha Action and Cut kimewahi kunipa tuzo kupitia muvi yangu ya Shikamoo Mzee.

 

Amani: Mpaka sasa umeigiza filamu ngapi?

JB: Sina takwimu sawasawa lakini zinachezea kwenye hamsini.

 

Amani: Unajivunia pia kipi kwenye tasnia hiyo?

 

JB: Kuonesha vitu vya tofauti na kukubalika zaidi. Lakini pia kuwaongezea vitu baadhi ya wasanii. Kwa mfano King Majuto alizoeleka kucheza muvi za vichekesho, lakini mimi nilimbadilisha na nikamchezesha muvi siriasi inayojulikana kwa jina la Nakwenda kwa Mzee. Pia Wema Sepetu, Muvi ya DJ Ben ilimfanya kumpindua Irene Uwoya ambaye kipindi hicho ndiye alikuwa na jina zaidi kwenye tasnia ya muvi. Jackline Wolper naye Muvi ya Taxi Dreva ilimfanya kupanda chati zaidi, hivyo hivyo kwa Aunt Ezekiel Muvi ya Signature.

MAKALA NA BONIFACE NGUMIJE, AMANI