Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia baada ya kutunuku vyeti vya pongezi na shukrani kwa wajumbe wa Kamati Maalumu za Uchunguzi na Majadiliano kuhusu Rasilimali za madini nchini katika hafla iliyofanyika Ikulu jijjini Dar es salaam leo Oktoba 23, 2017
Jonas Kamaleki- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewatunuku vyeti wajumbe wa Kamati za Madini leo Ikulu jijini Dar es Salaam ikiwa ni shukrani kwa kazi ya kizalendo waliyoifanya.Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli amesema kuwa watu hao wamefanya kazi kubwa na ya kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya watanzania hivyo wanastahili pongezi.Ninashukuru sana kwa kweli mmetengeneza ukurasa wa pekee kwani kazi mliyoifanya ni ya kujitoa sadaka,”alisema Rais Magufuli.Ameongeza kuwa watanzania wengi wanaunga mkono juhudi hizi za kulinda raslimali za taifa licha ya kuwepo watu wachache wanaobeza jitihada hizo na kusema hao inabidi wapuuzwe.Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa wameonyesha uzalendo kwa taifa ambalo lina raslimali nyingi lakini lilikuwa halifaidiki nazo bali zilikuwa zikiwafaidisha watu wachache.Rais amesema kuwa katika suala la kutetea na kulinda raslimali za nchi hasa madini, hakuna hata mahakama ambayo ingeinyima Serikali ya Tanzania ushindi kwani unyonyaji uliokuwa ukifanyika ulikuwa wa wazi, hivyo ameipongeza Kamati ya majadiliano chini ya Mwenyekiti wake, Prof. Paramagamba Kabudi.Amewataka watanzania kuwa na moyo wa kizalendo kwa kujali na kulinda raslimali za nchi bila kuangalia manufaa yao binafsi.Ningekuwa na ubinafsi mii ningekeuwa tajiri sana kwani nimefanya kazi katika Wizara ya Ujenzi kwa miaka 16, hivyo ningetaka kujitajirisha ningeweza, lakini hivyo vyote vya nini,” aliuliza Rais Magufuli.Katika makubaliano kati ya Tanzania na Barrick Gold Company Limited, mgawanyo wa faida itokanayo na madini utakuwa 50 kwa 50, jambo ambalo halifanyiki katika nchi yoyote ya Kiafrika, aliongeza Rais Magufuli.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya majadiliano upande wa Tanzania, Prof. Paramagamba Kabudi amesema kuwa Rais Magufuli anapaswa kupongezwa kwa msimamo wake katika suala zima la usimamizi wa raslimali za nchi hasa madini.Prof. Kabudi amenukuu magazeti ya Zambia jinsi yalivyompongeza Rais Magufuli kwa hatua hiyo. Amesema kuwa hakika nabii hakubaliki kwao, nje ya nchi wanampongeza Rais wakati baadhi ya watanzania wanabeza jitihada hizo.Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba amempongeza Rais magufuli kwa hatua anazozichukua katika kulinda raslimali za nchi na kuwataka wapinzani wenzie kumuuunga mkono.Mhe. Rais shikilia hapo hapo ili raslimali zetu ziweze kulindwa na kutunufaisha watanzania wote,”alisema Prof. Lipumba.Baadhi ya waliotunukiwa vyeti hivyo ni Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai, Prof. Paramagamba Kabudi, Prof. Abdulkadir Mruma, Prof. Nehemiah Ossolo, James Dotto, Dkt. Yamungu Kayandabila, Prof. Lwoga, Andrew Massawe, Prof. Rwezaula Ikingula, Dr. Ambrose Joseph na Prof. Longinus Lutasitara.Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mawaziri, Viongozi wa Dini, Viongozi wa vyama vya Siasa, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama,Wanahabari, na wageni wengine ambao walionyesha kufurahishwa na hatua za Serikali ya Awamu ya Tano katika kulinda raslimali za nchi.