Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mhe. January Makamba leo ameshiriki kwenye uzinduzi wa kongamano la vijana kuhusu Muungano viziwani Zanzibar, lenye lengo la kutambua fursa za kiuchumi na biashara zilizomo ndani ya muungano.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Waziri Makamba amewataka vijana walioshiriki kujadili kiupana kuhusu Muungano, kwakuwa vijana ndio watakaorithi uongozi siku za usoni.
“Mapinduzi yalifanywa ili kuipa Zanzibar Uhuru wa kujiamulia na kujifanyia mambo yake yenyewe na Muungano ulianzishwa ili kushirikiana na kuongeza fursa zaidi kati ya wananchi wa pande zote mbili. Tutambue kuwa maadui wa Mapinduzi na Muungano bado wapo na wataendelea kuwepo. Sisi tuliorithishwa inabidi tuulinde na tuhakikishe tunanufaika na fursa za uchumi zilizopo kwenye Muungano wenyewe,” amesema Waziri Makamba na kuongeza..
 
“…ustawi wa Zanzibar na vijana wake pamoja na matumaini waliyonayo juu ya mustakabali wao vina uhusiano wa moja kwa moja na utulivu wa Zanzibar na Muungano wenyewe. Kuwepo kwa changamoto hakupaswi kuwa sababu za kuuvunja Muungano wenyewe. Tutambue kuwa siku tatu tu baada ya Muungano kuanzishwa zilitokea changamoto, lakini waasisi hawakuamua kuuvunja Muungano – bali kuzitatua. Huu ndio unatakiwa kuwa mtazamo wetu kwenye kutatua changamoto zozote katika uhusiano kati ya pande mbili.”
 
“Hakukuwa na utarabu maalum wa kutoa ajira zinapotokea fursa za ajira kwenye taasisi za Muungano lakini tumehakikisha taasisi za Muungano zinafungua ofisi hapa Zanzibar na kuongeza nafasi kwa vijana wa hapa kuingia kwenye soko la ajira pale zinapotangazwa,” ameongeza Waziri Makamba na kufafanua juu ya usajili wa magari
 
“..tumeamua itungwe Sheria kwamba magari yatakayosajiliwa Zanzibar yatambuliwe kama yamesajiliwa Bara na vile vile ya Bara yatambuliwe Zanzibar.“amesema Waziri Makamba huku akimaliza kwa kumpongeza Rais Magufuli.
 
“Tunamshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa kutuamini na kutupa jukumu kubwa la kusimamia mambo ya Muungano lakini kufanikiwa kwake kunategemea sana mawazo na michango ya vijana ili sote kwa pamoja tushiriki kutafuta ufumbuzi wa changamoto za mambo yenye umuhimu mkubwa zaidi katika kuulinda Muungano wetu.”