Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam limelaani vikali mauaji ya kikatili ya askari wa jeshi hilo mwenye namba X-G 475 PC , Charles Yanga.

Akizungumza na waandishi wa habari leo hii, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Mambosasa amesema majira ya saa 12 asubuhi Ukonga jijini Dar es salaam askari wa jeshi hilo wakiwa kazini waliukuta mwili wa askari huyo ukiwa pembeni mwa uzio wa kambi ya Ukonga akiwa ameanguka chini huku pikipiki yake aliyokuwa akiendesha ikiwasha taa za tahadhari na  mwili huo ulikutwa ukiwa na majeraha kwenye paji la uso na sikio moja likiwa limekatwa kabisa.

Amesema polisi kupitia kikosi kazi chake kinaendelea na msako mkali wa ufuatiliaji wa tukio hili la kinyama ili kuwabaini watuhumiwa waliohusika kutekeleza mauaji hayo na kufikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka yanayowakabili. Katika hatua nyingine jeshi hilo limekiri kupokea malalamiko ya watu kupigwa na askari huku akidai vitendo hivyo haviendani na maadili ya jeshi la polisi.

“Jeshi la polisi, limepokea malalamiko ya watu wanaosemekana ni askari kufanya msako na kuwapiga wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na kambi ya Polisi kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) ambao hawana hatia yeyote. Jeshi la Polisi linalaani vikali vitendo hivyo ambavyo havina maadili ya kazi za Polisi”

Aidha jalada tayari limefunguliwa na uchunguzi unaendelea ili kuwabaini watuhumiwa wa tukio hilo, na kuomba wananchi watoe ushirikiano kutoa taarifa za wahusika ili kuwachukulia hatua watu au askari waliohusika na matukio hayo ya kuwapiga wananchi.