Ofisa Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jennifer Mushi akishuka ngazi baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili.
DAR ES SALAAM: Ofisa Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jennifer Mushi amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka mawili ikiwamo la kukutwa akimiliki magari 19, mali isiyolingana na kipato chake halali.
Jennifer ameshtakiwa chini ya kifungu cha 27, (1) (a) na (b) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11ya mwaka 2007.
Akisoma hati ya mashtaka leo Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alidai kuwa mshtakiwa huyo kati ya Machi 21,2016 na Juni 30, 2016 jijini Dar es Salaam akiwa mwajiriwa wa TRA kama Afisa Forodha Msaidizi alikutwa akimili magari 19.
Nagari hayo ni Toyota RAV4, Toyota RAV4, Toyota Dyna Truck, Toyota Viz, Suzuki Carry, Toyota Ipsum, Toyota Wish, Toyota Mark II, Toyota Wish na Toyota Mark X.
Mengine ni Toyota Regiusage, Toyota Estimated, Toyota Alex, Toyota Noah, Toyota Crown, Toyota Hiace, Toyota Estima, Toyota Passo na Suzuki Carry yote yakiwa na thamani ya Sh 197,601,207 Mali ambayo hailingani na kipato chake halali.
Wakili huyo wa Serikali Mkuu, Vitalis alidai kuwa mshtakiwa huyo kati ya Machi 21 ,2012 na Machi 30, 2016 Dares Salaam akiwa mwajiriwa wa Mamlama ya Mapato Tanzania (TRA) kama Afisa Forodha Msaidizi alikutwa akiishi maisha ya kifahari yenye thamani ya Sh 333,255,556.24 fedha ambayo hailingani na Kipato chake halali.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo mshtakiwa huyo alikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo imekamilika.Wakili wa mshtakiwa huyo, Elisaria Mosha aliiomba Mahakama kumpatia dhamana mteja wake ya masharti nafuu.
Hakimu Shaidi, alimtaka mshtakiwa huyo kuwa nmdhamini mmoja anayeaminika ambaye alisaini bondi ya Sh. 20 milioni.
Aidha mtuhumiwa huyo alikamilisha masharti hayo ya dhamana na kuachiwa huru.
Kesi imeahirishwa hadi Novemba 7,mwaka huu kwa, ajili ya mshtakiwa huyo kusomewa maelezo ya awali (PH).