Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufungua kambi ya uchunguzi wa macho, kisukari na shinikizo la damu.Kambi hiyo ya siku tatu imeandaliwa kwa pamoja kwa kushirikiana na Klabu ya Lions ya Dar es Salaam (Host), kwa kushirikiana na Hospitali ya Regency ya jijini hapa.Kambi hiyo itakuwa bure kwa wananchiwote watakaojitokeza kuanzia siku ya Ijumaa katika Wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Lions Klabu iliyotolewa na Mwenyekiti wa Hospitali ya Regency Dk. Rajni Kanabar, ufunguzi rasmi wa kambi hiyo utafanyika siku ya Jumamosi na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Kambi hiyo itafanyikia kwenye kiwanda cha KNAUF Gypsum Wilaya ya Mkuranga, Kata ya Vikindu kijiji cha Kisemvule Mkoa wa Pwani kuanzia siku ya Ijumaa wiki hii.
Alisema kambi hiyo ya bure ya siku tatu itaanza tarehe 27 hadi 29 mwezi huu
Dk. Rajni Kanabar, aliwataka wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam na Pwani kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo.
Alisema Lions Klabu ya Lions imeamua kuandaa kambi hiyo ya bure baada ya kubaini kuwa kuna wananchi wengi wanasumbuliwa na maradhi hayo lakini wanakosa uwezo wa kwenda kupima.
“Hii ni fursa adimu watu wajitokeze kwa wingi kuja kupima afya zao bure, huduma hiii itatolewa kwa muda wa siku tatu mfululizo kuanzia siku ya Ijumaa hadi Jumapili hivyo wananchi wote wachangamkie hii fursa,” alisema.
Klabu ya Lions ya Dar es Salaam (Host), imekuwa ikiandaa kambi ya uchunguzi mbalimbali kila mwaka ambapo wananchi hupata fursa ya kwenda kupima bure.