Uhuru Kenyatta.
RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ameombwa kutia sahihi mara moja Miswada ya (Marekebisho) wa Sheria ya Uchaguzi inayohusu uchaguzi ulipoangwa kufanyika kesho nchini humo.
Wakizungumza kutoka Addis Ababa, Ethiopia, wajumbe wa umoja wa wanasiasa wa upande wa Jubilee unaomuunga mkiono rais huyo, wamemwomba asaini miswada hiyo kuwa sheria ili kusaidia kujenga mazingira mazuri kwa ajili ya uchaguzi wa rais utakaorudiwa Alhamisi wiki hii.
Likiongozwa na Mbunge wa zamani wa Budalangi, Ababu Namwamba, Baraza la Wataalam la Kenya (CPK)lililo upande wa Jubilee, lilimshauri rais huyo kusaini miswada hiyo ili iwe kinga ya uchaguzi huo wa Oktoba 26 kutofutwa tena.
CPK imetahadharisha kwamba bila ya marekebisho hayo ya sheria, nchi itatumbukia katika mgogoro mkubwa zaidi wa kikatiba iwapo matokeo ya uchaguzi huo yatafutwa tena. Kundi hilo limeutaka upande wa umoja waNational Super Alliance (NASA) kuacha kuishambulia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na wafanyakazi wake.

“Tunatoa wito kwa upinzani kuheshimu kanuni za uchaguzi wa ushindani kama msingi wa demokrasia na uhakikisho pekee wa amani na utulivu wa kidemokrasia. Wakenya wote wana haki ya kupiga kura bila ya vitisho,”ilisema sehemu ya taarifa ya Namwamba.

Profesa Peter Kagwanja, aliyetoa taarifa hiyo kwa niaba ya Namwamba, alifichua kwamba ujumbe huo ulikuwa umefanya ziara makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) ili kufungua mashitaka dhidi ya kiongozi wa NASA, Raila Odinga, ukidai anataka kuleta machafuko nchini Kenya.