Tende ni tunda lenye ladha tamu na nzuri mdomoni , lakini kisayansi pia limethibitika kusheheni madini na vitamini lukuki, hivyo kuwa na faida nyingi kiafya.

1 .Ukila tende mara kwa mara , mwili wako utapata aina mbalimbali za madini na vitamin za kutosha, ambazo zinapatikana kwenye tunda hili maarufu duniani na katika tende kuna kiasi kidogo tu cha mafuta (fat) na haina lehemu(kolestrol) .

2 .Unaweza kujipatia kiasi cha kutosha cha protini na vitamin B1, B2, B3, B5, A1, na C, virutubisho ambavyo ni muhimu kwa ustawi wa afya ya mwili wako kwa ujumla .

3 . Ulaji wa tende huimarisha na kuboresha mfumo wa usagaji chakula tumboni, hivyo utaondokana na matatizo ya ukosefu wa choo, au matatizo ya kupata choo kigumu kinachosababisha maumivu wakati wa kujisaidia . Pia ndani ya tende kuna virutubisho vya ‘ amino acids’ ambavyo ni muhimu mwilini .

4 .Ukila tende, mwili utapata nguvu na kukuondolea uchovu ndani ya nusu saa tu, kwa sababu tende ina virutubisho vya sukari asilia kama vile ‘glucose ’ ‘sucrose’ na ‘fructose’. Ili kupata faida zaidi za tende, changanya na maziwa fresh kisha kula. Unapojisikia mchovu, badala ya kunywa vinywaji baridi vinavyodai kuongeza nguvu , kula tende, hata kiasi cha punje tatu kinatosha .

5 . Kwa wale wenye matatizo ya ugonjwa wa kukauka damu mwilini wanaweza kupata ahueni kwa kula tende kwa wingi ambayo ina kiwango cha kutosha cha madini ya chuma ambayo huhitajika katika utengenezaji wa damu mwilini , wakati vitu vitamu vingine huozesha meno, utamu wa tende huzuia uozaji wa meno.