Kenyatta na Odinga.
WANANCHI wa Kenya wanatarajia kushiriki katika uchaguzi wa rais leo, huku hali ya utulivu ikiendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki baada ya kukamilika kwa kampeni za uchaguzi.Taarifa iliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inasema kuwa, maandalizi ya uchaguzi huo yamekamilika huku vyombo vya usalama vya Kenya vikitangaza kwamba, vimejiandaa kikamilifu kwa ajili ya kusimamia zoezi la uchaguzi huo ili lifanyike kwa amani.
Karatasi ya kupigia kura yenye majina ya wagombea.
“Vituo vya kupiga kura vitafunguliwa kuanzia saa 12 asubuhi kesho (leo) na Rais Uhuru Kenyatta atapiga kura kwenye Shule ya Msingi Mutomo iliyoko Gatundu South, Kiambu. Shule hiyo imeelezwa kukarabatiwa siku chache zilizopita ili iwe na muonekano mzuri na kwa heshima ya kiongozi huyo,” imesema IEBC.
Raia akipiga kura.
Mpinzani mkuu wa Uhuru, Raila Odinga anayegombea kupitia muungano wa vyama vya upinzani (NASA), alijiandikisha kupiga kura kwenye eneo la Kibra, jijini Nairobi japokuwa ameshatangaza kujitoa.
Mshindi wa kiti cha urais anapaswa kupata asilimia 50+1 ya kura. Uchaguzi wa mara hii nchini Kenya unatajwa kuwa na ushindani mkubwa huku kukiwa na wasiwasi wa kuibuka machafuko katika baadhi ya maeneo na kuna taarifa kuwa baadhi ya watu wameyahama makazi yao wakihofia usalama wa maisha yao.