Mbunge wa Ilala, Dar es Salaam, Mussa Azzan Zungu, amefika eneo la Jangwani na kujionea maji yalivyofulika kwenye eneo la Daraja na njia yote jambo ambalo limesababisha kukata mawasiano ya njia Barabara ya kawaida na mwendo kasi.

Akizungumza na waandishi wa habari amesema mvua ni kubwa na maji yanaendelea kujaa hivyo wananachi na Serikali wasaidiane ili waweze kunusuru maisha ya watu haswa wale wanaopita kwa kutumia njia hiyo na wakazi walioko karibu na Jangwani.

“Kama tunavyoona nyumba nyingi zimefunikwa na maji na hadi sasa tunangoja gari yani kijiko kiweze kufika hapa na kusaidia kupunguza maji katika maeneo haya”amesema

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema hakuchelewa kufika katika eneo hilo na kuzungumza na waandishi ambapo amesema mvua zitaendelea kunyesha hadi jumamosi kwa mujibu wa mamlaka ya hali ya hewa.

“Tunaomba Wananchi wachukue tahadhari na hizi mvua kwani bado zinaendelea kunyesha lakini wazazi wawe makini na watoto wao ikiwezekana wawaache nyumbani wasiende shule hadi mvua hizi ziishe ili tusije kupoteza watoto wanaosoma shule za kupitia njia hii ya jangwani” amesema Mjema

Aidha amewataka wananchi wanaokaa maeneo hayo waondoke kama wana ndugu zao waende kuishi huko kuliko kulala pale kwani matatizo makubwa yanaweza kutokea.