KESI YA LULU: Wazee wa Baraza: “Lulu ameuwa bila kukusudia” Mahakama Kuu ya Tanzania inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya kuuwa bila kukusudia inayomkabili Elizabeth Michael ‘Lulu’ November 13, 2017. Hatua hiyo inatokana Wazee watatu wa Baraza kutoa ushauri wao kwa mahakama kwamba Lulu’ ameua bila kukusudia. Lulu anakabiliwa na kesi ya kuuwa bila kukusudia, ambapo anadaiwa kumuuwa Msanii mwenzake marehemu Steven Kanumba, April 7, 2012. Awali, kabla ya wazee kutoa maoni hayo, Jaji Sam Rumanyika alisoma maelezo ya ushahidi wa pande zote mbili kisha kusikiliza maoni hayo.

 

        Kabla ya kutoa maoni hayo, Jaji Rumanyika alisema kimsingi ushahidi wa upande wa mashtaka umejikita kwenye ushahidi wa kimazingira kwa sababu Lulu ndiye mtu wa mwisho kuwa na Kanumba. Alisema kuwa ushahidi wa kimazingira unakuwa sio wa moja kwa moja, licha ya kuwa una vipande mithili ya nyololo ambavyo vimeshikana. “Hivyo waungwana mkumbuke katika utoaji wa maoni yenu sio lazima mthibitishe makosa, pia kama mkiona mshtakiwa hausiki basi msisite kuieleza mahakama,”. Akitoa maoni yake, Mzee wa Baraza Omary Panzi amesema Lulu ameua bila kukusudia.

 

Amesema kuwa hatua hiyo inatokana na ushahidi wa mdogo wake Kanumba, Seth Bosco ambaye alielezea ugomvi uliotokea baina ya Lulu na marehemu. >>>”Maoni yangu ni kwamba marehemu alikufa kwa sababu ya kuteleza ikizingatiwa ilikuwa ni usiku na kulikuwa na giza, na chanzo cha kutekeleza ni ugomvi wake na Lulu.” Pia Mzee wa pili, Bi. Sarah amesema Kanumba alikufa kutokana na ugomvi ambapo ushahidi pia umetueleza kulikuwa na Giza.

 

Hivyo Lulu hakuua makusudi bali aliuwa bila kukusudia.” Naye Mzee wa Tatu, Rajabu Mlawa ametoa maoni yake akisema kutokana na sababu zilizosomwa anaridhika na hakuna ubishi kuwa Lulu ana kosa la kuua bila kukusudia. >>>”Ameuwa bila kukusudia na nimeridhika na kilichosemwa, kwani Kanumba alikuwa na mwili mkubwa na alikuwa katika hali ya kulewa, hivyo inaonekana katika heka heka za ugomvi inawezekana Lulu alitumia nguvu kidogo ya kumsukuma Kanumba hadi kudondoka.” Baada ya kutoa maoni hayo, Jaji Rumanyika amesema kuwa anatarajia kutoa hukumu ya kesi hiyo November 13, 2017.