Mshambuliaji na nahodha waTaifa Stars na klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji amefunga bao moja wakati timu yake ikipata ushindi wa 2-0 dhidi ya Vinara wa Ligi hiyo Club Brugge kwenye uwanja wao wa nyumbani Luminus Arena. Samatta amefunga goli lake dakika ya 90 na kumaliza wimbi la kucheza bila kufunga ambapo alishacheza mechi tisa bila kutupia kabambani kabla ya kuwafunga Brugge, bao la kwanza la Genk limefungwa na Ruslan Malinovskiy dakika ya 43 kipindi cha kwanza.

 

     Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Genk katika mechi tano zilizopita, kabla ya ushindi huo waliwafunga Anderlecht 1-0 ugenini. Matokeo ya Genk katika mechi tano zilizopita Genk 1-1 KV Oostende AS Eupen 3-3 Genk Genk 1-1 Royal Excel Mouscron Anderlecht 0-1 Genk Genk 2-0 Club Brugge Timu ya Club Brugge ndio vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 30, kipigo kutoka kwa Genk ni cha pili kwao wakiwa wamesha cheza mechi 12 wameshinda 10 na kupoteza michezo miwili hawajatoka sare hata mechi mmoja.

 

Ushindi wa Genk dhidi ya Brugge unawafanya wafikishe pointi 17 baada ya kucheza mechi 12 na wamepanda hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi. Katika mechi 12 ambazo Genk wamecheza, wameshinda nne, sare tano huku wakipoteza mechi tatu. Wamefunga magoli 20 huku wenyewe wakiwa wameruhusu kufungwa magoli 17 hivyo kufanya wastani wa magoli kuwa ni tatu. October 28, 2017 Genk watakuwa ugenini kucheza dhidi ya Kortrijk mchezo wa ligi kuu ya Ubelgiji.