IKIWA ni wiki moja sasa tangu Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ianze kusikiliza mfululizo kesi inayomkabili muigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’, wazee wa Baraza la mahakama hiyo leo Oktoba 26, 2017 wametoa maoni yake kuwa Lulu alimuua Kanumba bila kukusudia. Katika maoni hayo yaliyotolewa na Jopo la Wazee watatu wa mahakama kwa nyakati fofauti, wote wamesema Lulu alimuua msanii mwenzake huyo bila kukusudia.

 

    Awali kabla ya kutoa maoni yao, Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Sam Rumanyika, aliwakumbusha wazee hao na mahakama kwa ujumla kuhusu maoni mbalimbali ya ushahidi wa pande zote mbili (utetezi na mashtaka) ambao tayari umeshawasilishwa na kusikilizwa mahakamani hapo. Hatua hiyo ya wazee kutoa maoni yao imekuja baada yakusikilizwa kwa ushahidi upande wa Jamhuri na upande wa utetezi ambapo jana yalisomwa mahakamani hapo maelezo ya mke wa Dkt. Slaa, Josephine Mshumbusi, aliyekuwa daktari wa marehemu Kanumba enzi za uhai wake. Jaji Rumanyika ameiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 13 mwaka huu ambapo Mahakama hiyo itatoa hukumu.