MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa mshtakiwa Harbinder Sethi pamoja na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH) na kuchukuliwa vipimo bado hajapata majibu wala matibabu yoyote na afya yake inazidi kuzoofika.

Wakili wake, Alex Balomi leo ameeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi Mara baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine.

Kishenyi baada ya kueleza hayo, Wakili Balomi alieleza kuwa kwa kiasi fulani upande wa Mashtaka umetekeleza amri ya mahakama kwa kumpeleka Muhimbili na kuchukuliwa vipimo lakini hajapewa majibu na wala hajatibiwa hadi sasa.

Amedai kuwa lile puto alilowekewa tumboni Sethi linatakiwa kubadilishwa mwishoni kwa mwezi huu, lisipobadilishwa litageuka kuwa sumu na kuhatarisha uhai wake.
Aliendelea kudai kuwa daktari aliyechukua vipimo ampatie majibu ili aweze kujua hali ya afya yake ikoje.

Wakili Kishenyi baada ya kutolewa kwa maelezo hayo alidai kuwa wao wamekwisha tekeleza amri ya mahakama, hawana cha kufanya zaidi kwa sababu majibu ni siri ya magonjwa na Daktari.

Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Takukuru, Leonard Swai yeye naye alidai kuwa suala la majibu ni suala la magonjwa na Daktari.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Shaidi Alisema amri ya mahakama imetekelezwa ambapo mshtakiwa alipelekwa Muhimbili, na siyo jukumu la mahakama kuingilia kazi ya Daktari hivyo alishauri mawakili wa upande wa utetezi wafuate utaratibu.

Kesi imeahirishwa hadi Novemba 10,2017 kwa ajili ya kutajwa na kuusisitiza upelelezi ukamilishwe.