Mjini mtu atakunyima tonge la ugali lakini siyo ubuyu! Madai mazito yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii yananyetisha kuwa, mwanamama mjasiriamali wa Afrika Mashariki, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ameibua utata mkubwa kuwa huenda amenasa mimba tena ya mtoto wake wa sita.

Kwa mujibu wa kundi linalojiita Team Zari, kwa upande wao ni furaha tupu baada ya yeye mwenyewe kuonesha kuwa amepewa sharti la kupumzika na daktari kwa kipindi chote cha ujauzito wake huo mpya.

Mbali na Team Zari, chanzo cha karibu cha familia ya mzazi mwenza wa mwanamama huyo ambaye ni msanii wa Bongo Fleva kililiambia Ijumaa Wikienda kuwa, Zari alikuwa amepanga tangu awali kuhusu watoto wake atakaozaa na jamaa huyo na namna watakavyopishana na wale wengine wawili, Tiffah na Dylan.

“Ni vigumu kuamini lakini huo ndiyo ubuyu wa mjini. Zari sasa hivi ana ujauzito mwingine. Ni jambo alilopanga kabisa maana alitaka kuzaa kama alivyomzaa Tiffah na mdogo wake, Dylan na alipanga kumzalia mzazi mwenzake huyo watoto watano,” kilisema chanzo hicho.

Mpashaji wetu huyo aliongeza kuwa, kama ukitaka kujua ukweli hata ukiangalia posti mbalimbali za Zari kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Snap Chat ameanza kutundika picha mbalimbali akiwa ameshika tumbo huku akiweka ujumbe ambao unaashiria kuwa tayari amenasa ujauzito mwingine.

“Unajua watu wanaona kama utani kama ilivyokuwa kwa Dylan, lakini hiyo ndiyo huwa ni staili ya Zari maana hata ukiwatazama wale watoto watatu wa kiume (aliozaa na mumewe wa awali, marehemu Ivan Ssemwanga),” alisema sosi huyo.

Ijumaa Wikienda lilizungumza na mmoja wa wanafamilia wa msanii huyo wa Bongo Fleva aliyefunguka kwamba, kuhusu suala la watoto, Zari anataka kuweka rekodi ya kuzaa watoto 12 ‘dazeni’ kwa wanawake wa kizazi hiki ambao jambo hilo ni gumu mno.