Mkurugenzi wa Swahili Fashion Week, Mustapha Hassanali akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa nembo ya miaka 10 ya wiki ya maonyesho ya mitindo ya ‘Swahili fashion week and Awards’, yatakayofanyika kuanzia Desemba 1 hadi 3 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa wa Basata, Vivian Shalua akizungumza na waandisishi wa habari na kuzindua wiki ya maonyesho ya mitindo ya ‘Swahili fashion week and Awards’ yatakayofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Swahili Fashion Week, Mustapha Hassanali na kulia ni Mkurugenzi wa Uzalishaji Vipindi wa Azam TV, Charles Hillary.

Baadhi ya wanamitindo wakifuatilia jambo kwenye mkutano wa uzinduzi wa nembo ya miaka 10 ya wiki ya maonyesho ya mitindo ya ‘Swahili fashion week and Awards’ yatakayofanyika jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa wa Basata, Vivian Shalua akizindua nembo ya miaka 10 ya wiki ya maonyesho ya mitindo ya ‘Swahili fashion week and Awards’ leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa wa Basata, Vivian Shalua akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Swahili Fashion Week, Mustapha Hassanali pamoja na baadhi ya wanamitindo wa hapa nchini.

Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii.
Baraza la Sanaa la Taifa nchini, leo Novemba 1, limezindua nembo ya miaka 10 ya wiki ya maonyesho ya mitindo ya ‘Swahili fashion week and Awards’, yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Desemba 1 hadi 3 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa wa Basata, Vivian Shalua amesema maonyesho hayo yanalenga kuinua uchumi wa nchi, kukuza lugha ya Kiswahili na kupanua fursa ya masoko Tanzania na Afrika Mashariki.

Aidha, Shalua amesema, maonyesho hayo ya mitindo ni moja ya maonyesho yanayozalisha ajira za kudumu na hata za muda na pia kuzalisha pato na kuongeza fedha za kigeni kwa kuuza nguo nje ya nchi.

“Nawapongeza sana waandaji wa maonyesho ya mitindo ‘Swahili Fashion week and Awards’ kwani ni mashindano pekee ambayo hayajawahi kusimama hata mara moja tangu kuanzishwa kwake mwaka 2008” amesema Shalua.

Aidha amewaasa wanamitindo wote ambao wanafanya kazi zao kinyemela bila ya kupitia Basata kwa minajili ya kukwepa kulipa kodi mwisho wao umefika, waache mara moja kwani serikali hii ya awamu ya tano haitawaacha bure.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Swahili Fashion Week na mbunifu mbunifu mkongwe, Mustapha Hassanali amesema maonyesho haya ya Swahili fashion week yatasaidia kutekeleza pia juhudi za Rais Pombe Magufuli katika sera ya kuwa na Tanzania ya uchumi wa viwanda kupitia bidhaa za nguo zinazotengenezwa nchini.

Amesema, hatua hii kubwa ya kusherehekea miaka kumi itaendelea kuwa kivutio katika maonyesho yote ya mitindo nchini Tanzania huku wabinifu wa ndani na wale wakimataifa wakipata hisia za dhati kwani Swahili fashion week ni jukwaa la kwanza lenya ubunifu kwa wabunifu wa mitindo Africa nzima kwa kuonyesha mavazi yao ulimwenguni kote.

Amesema, maonyesho ya Swahili week mwaka huu yatafanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa kuanzia tarehe 1-3 Desemba na pia yatakuwa na wabunifu zaidi ya 50 kutoka nchi mbali zikiwemo, Nigeria, Malawi, Kenya, Uganda, Kenya na nyinginezo ambapo wajasiliamali watapata fursa ya kuonyesha kazi zao za mikono.

“Tunaomba wadau wajitokeze kwa wingi kusherehekea nasi siku hii muhimu kwa kuwaunga mkono wabunifu wetu wa mitindo vile vile watashuhuhudia mitindo ya kipekee katika maonyesho haya”, amesema Hassanali

Kwa upande wake, Meneja mradi wa Swahili Fashion Week, Glory Urrasa amesema katika sherehe hizo, wanakazania kuboresha sekta ya ukuaji wa mitindo kwa Africa Mashariki wananchi wakishuhudia ukuaji mzuri wa wabunifu wa mitindo,

“Tofauti na miaka iliyopita, maonyesha haya ya kumi yanajumuisha na utoaji wa tuzo katika siku zote tatu za maonyesho huku tukisisitiza jamii kuwa mitindo ni pato linalozalisha tasnia ya ubunifu na kukuza dhana ya bidhaa za Africa. amesema Urrasa.