Vifaranga vya kuku 6,400 vilivyokamatwa mpakani Namanga wilayani Longido mkoani Arusha vikiingizwa nchini kutoka Kenya Jumapili Oktoba 29,2017 vimeteketezwa. Vifaranga hivyo vyenye thamani ya Sh12.5 milioni ni mali ya mfanyabiashara Mary Matia (23) mkazi wa Mianzini jijini Arusha. Uteketezaji wa vifaranga hivyo umefanyika leo Jumanne Oktoba 31,2017 katika eneo maalumu mpakani Namanga.
 Kazi ya kuviteketeza imefanyika ikishuhudiwa na maofisa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Wizara ya Mifugo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na vyombo vingine vya ulinzi na usalama. Akizungumza wakati wa kuteketeza vifaranga hivyo, ofisa mfawidhi wa kituo cha udhibiti wa magonjwa ya mifugo Kanda ya Kaskazini, Obedi Nyasebwa amesema kazi hiyo imefanyika kwa kuzingatia Sheria ya Magonjwa ya Wanyama namba 17 ya maka 2003. Pia, amesema Serikali mwaka 2007 ilitoa tangazo kupiga marufuku kuingizwa nchini vifaranga vya kuku na mayai.
“Tumevichoma vifaranga ili visisambazwe nchini kwa kuwa hatujui usalama wake na hasa kutokana na kuwepo taarifa za ugonjwa wa mafua ya ndege nchi jirani,” amesema. Mmiliki wa vifaranga hivyo, Matia ambaye bado anashikiliwa na polisi pamoja na gari lake aina ya Toyota Hiace amesema amepata hasara kubwa.
“Nimewaomba tuvirejeshe Nairobi, Kenya nilikovinunua wamegoma, sikuwa najua kama ni makosa kununua viranga nchini Kenya,” amesema. Amesema ni mfugaji wa kuku na amekuwa akiwauza. Matia amesema vifaranga hivyo vyenye thamani ya Sh12.5 milioni alivinunua ili kuvikuza na kuuza. “Nimepata hasara kubwa, nilikuwa nimekopa fedha sijui nitarudisha vipi,” amesema.
Chanzo: Mwananchi