Waziri wa Nishati wa Tanzani, Dkt. Medard Kalemani (kulia) na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Nishati kutoka nchini Uganda, Dkt. Simon Du’ Ujanga wakitia saini ripoti ya mkutano huo. Wanaoshuhudia wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki upande wa Sekta za Kijamii na Uzalishaji, Christophe Bazivamo na wawakilishi wa Mawaziri wa nchi wanachama.

Makatibu Wakuu wa nchi wanachama wakisaini ripoti iliyojadiliwa katika mkutano huo. Kwa upande wa Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Nishati kutoka Wizara ya Nishati James Andilile amemwakilisha Katibu Mkuu Wizara hiyo.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akizungumza jambo wakati wa mkutano huo. Wanaomsikiliza ni ujumbe wa Tanzania ulioshiriki Mkutano huo.

Sehemu ya Washiriki wa Mkutano huo kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akisalimiana na Wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi mbalimbali zinazohusika na Masuala ya Nishati na Zanzibar baada ya kukamilika kwa mkutano.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (wa kwanza kulia) akiwa na Wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) mara baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mbele, washiriki kutoka nchi ya Rwanda wakiwa katika Mkutano huo.

Waziri wa Nishati wa Tanzani, Dkt. Medard Kalemani (kulia) na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Nishati kutoka nchini Uganda Dkt. Simon Du’ Ujanga wakitia saini ripoti ya mkutano huo.

………………………………………………………………………………..

Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki ulioanza tarehe 30 Oktoba, 2017 Makao Makuu ya Jumuiya hiyo Jijini Arusha, umehitimishwa leo na Kikao cha Mawaziri wa nchi Wanachama.

Kikao cha Mawaziri kilitanguliwa na Vikao vya Wataalam wa Sekta ya Nishati , Kikao cha Kamati ya Nishati ya Baraza hilo na Kikao cha Makatibu Wakuu wa nchi husika.

Katika kikao cha Mawaziri, viongozi hao pia wametia saini ripoti iliyojadiliwa katika vikao hivyo ambapo masuala kadhaa yakiwemo ya miradi ya Umeme ya mipakani, miradi ya umeme ya nchi na nchi, Mafuta, Gesi , Nishati Jadidifu , Sera ya Usalama wa Nishati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na mambo mengine yalijadiliwa.

Awali, kabla ya Mawaziri wa nchi wanachama kutia saini ripoti hiyo, pia ilisainiwa na Makatibu Wakuu wa nchi wanachama.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki upande wa Sekta za Kijamii na Uzalishaji, Christophe Bazivamo ameeleza umuhimu wa kikao cha Mawaziri na kueleza kuwa, ndiyo kikao ambacho kinatoa mwelekeo wa utekelezaji wa yale yanayokubaliwa na nchi wanachama. Aidha, Bazivamo ameendelea kusisitiza kuhusu umuhimu wa nishati kwa ajili ya maendeleo ya nchi jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye ni Waziri wa Nchi anayeshughulikia Nishati kutoka nchini Uganda, Dkt. Simon D’ Ujanga, amesema kuwa, Viongozi wa nchi zote za Jumuiya hiyo wanayo nia ya kuhakikisha kwamba miradi iliyokubaliwa na jumuiya inatekelezwa, Pia amewataka nchi wanachama

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewashukuru wataalam wote ambao wamefanikisha kukamilika kwa ripoti ambayo itawezesha makubalino yaliyofikiwa kutekelezwa na jumuiya hiyo na kuongeza kuwa, yote yaliyojadiliwa katika mkutano huo yanagusa nchi zote na hivyo yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito.

Nchi zilizoshiriki mkutano huo ni Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi. Aidha, Mwenyekiti wa mkutano huo ilikuwa nchi ya Uganda na Katibu nchi ya Rwanda.

Tanzania katika mkutano husika imewakilishwa na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maji, Mazingira na Nishati ya Zanzibar, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Wakala wa Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta , Zanzibar (ZURA).