Msanii wa muziki Bongo Fleva mwenye mafanikio makubwa nchini Tanzania, Naseeb Abdul, maarufu kwa jina la kisanii ‘Diamond Platinumz’ ameeleza kuwa licha ya kuupenda muziki, ari ya kutaka kuuonyesha umma kwamba muziki unaweza kuwa msaada kwa jamii ndiyo sababu iliyomsukuma kuingia katika tasnia hiyo.Diamond ameyaeleza hayo alipokuwa akifanya mahojiano na mtangazaji, Salim Kikeke, wa kituo cha kurusha matangazo cha Uingereza, BBC ambapo ameeleza kuwa lengo lake ni kutaka kuwafumbua akili vijana kuwa muziki unaweza kutumika kutengeneza fursa mbalimbali pamoja na kuwa chanzo cha mapato.Napenda kuutumia muziki kwa njia nzuri, kuwaonyesha vijana wenzangu kama unaweza kuwa mwanamuziki na ukautumia katika misingi bora ukatengeneza ajira, ukatengeneza kitu ambacho kitakusaidia hata utakaposhindwa muziki,” alisema Diamond.
Vilevile Diamond alieleza kuwa yuko mbioni kuachia albam yake mpya ambayo amewashirikisha wasanii kutoka nchi mbalimbali duniani huku akitaja wimbo mpya wenye jina ‘Waka’ aliomshirikisha msanii kutoka nchini Marekani ‘Rick Ross’ ma kusema kuwa utatoka Disemba mosi, mwaka huu.

Mbali na muziki, Diamond ameeleza kuwa anajihusisha na biashara nyingine ili aweze kujiingizia kipato na kuendesha maisha yake. Biashara alizozitaja ni pamoja na ‘Diamond Karanga’ na ‘Chibu Perfume’ ambazo zimejipatia umaarufu mkubwa sana hapa nchini.