Mhandisi Khalid Songoro wa kandarasi ya Songoro Marine Transport Boatyard akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye mchoro wa meli mpya inayojengwa na kampuni hiyo kwa ajili ya kusafirisha abiria na mizigo kwenye mwambao wa ziwa Nyasa wakati wa ziara yake kwenye bandari ya Itungi iliyopo Kyela mkoani Mbeya.

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) akikagua muonekano wa mpya inayojengwa na kandarasi ya Songoro Marine Transport Boatyard kwa ajili ya kusafirisha abiria mia mbili na mizigo tani mia mbili kwenye mwambao wa ziwa Nyasa wakati wa ziara yake kwenye bandari ya Itungi iliyopo Kyela mkoani Mbeya.

Kapteni wa meli Bwana Noel Madete akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye vifaa vya kisasa vya uendeshaji wa meli vilivyopo kwenye meli ya mizigo ya MV Njombe wakati wa ziara yake kwenye bandari ya Kiwira iliyopo wilayani Kyela mkoani Mbeya. Anayeshuhudia aliyevaa koti ni Meneja wa bandari za ziwa Nyasa Bwana Ajuaye Msese.

Muonekano wa meli ya mizigo ya MV Njombe inayosafirisha mizigo ndani ya ziwa Nyasa kwa wateja wa ndani na nje ya nchi ikiwa kwenye bandari ya Kiwira iliyopo wilaya ya Kyela mkoani Mbeya baada ya kukaguliwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) wakati wa ziara yake bandarini hapo.

Muonekano wa meli ya MV Songea iliyopo bandari ya Itungi, Kyela mkoani Mbeya baada ya kukaguliwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) ambayo itafanyiwa tathmini ya gharama za matengenezo na Songoro Marine Transport Boatyard kwa ajili ya kukarabatiwa na ili ianze kutoa huduma za usafirishaji.

Serikali inajenga meli mpya ya kusafirisha abiria na mizigo ambapo ujenzi wake unagharimu shilingi biloni tisa kwa ajili ya bandari za Ziwa Nyasa ambapo itatoa huduma kwa wananchi waishio eneo la mwambao wa bandari za Ziwa Nyasa.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo kwenye bandari ya Itungi iliyopo wilayani Kyela mkoani Mbeya yenye uwezo wa kubeba abiria mia mbili pamoja na mizigo tani mia mbili.

Wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo kwa Mhandisi Nditiye, Meneja wa Bandari za Ziwa Nyasa Bwana Ajuaye Msese amesema kuwa ujenzi wa meli hiyo umegharimu kiasi cha gharama ya shilingi bilioni tisa na umekamilika kwa kiwango cha asilimia sabini ambapo ujenzi wake ulianza mwezi Julai mwaka 2017 na utakamilika mwezi Juni mwaka huu.

Ameongeza kuwa meli hiyo itaanza kutumika mwezi Agosti mwaka huu na itafanya safari zake kwenye bandari za ziwa Nyasa kwa wananchi wa mwambao wa ziwa hilo kuanzia bandari ya Itungi iliyopo wilayani Kyela mkoani Mbeya hadi Bamba bay, Malawi. Msese amesema kuwa meli hiyo inajengwa na mkandarasi mzawa wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Boatyard.

Mhandisi Nditiye amesema kuwa Serikali imetoa fedha kujenga meli hiyo mpya ili kutimiza ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambayo ameitoa kwa wananchi waishio kwenye mwambao wa ziwa Nyasa. “Ni matarajio ya Serikali kuwa meli hii itainua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla, itaondoa changamoto ya usafiri, itapunguza gharama ya usafiri kwa kuwa usafiri wa meli ni wa gharama nafuu sana, hivyo nitoe rai kwa wafanyabiashara watumie meli hii kusafirisha mizigo yao”, amesema Mhandisi Nditiye.

Pia amelielekeza Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kufunga mitambo ya kisasa ya mawasiliano kwenye meli hiyo ili abiria wapate mawasiliano muda wote ndani ya meli wakiwa safarini ndani ya ziwa Nyasa na nchi za jirani za Malawi na Msumbiji ambapo meli hiyo itatoa huduma ya usafiri.

Katika ziara hiyo wilayani Kyela, mkoani Mbeya, Mhandisi Nditiye amekagua meli mpya za kisasa za MV Njombe na MV Ruvuma kwa ajili ya kubeba mizigo zilizopo kwenye bandari ya mizigo ya Kiwira. Bwana Msese amesema kuwa meli hizo zimeanza kazi ya kusafirisha mizigo ndani na nje ya nchi na ni maalumu kwa ajili ya kubeba mizigo tu ambapo kila moja ina uwezo wa kubeba mizigo yenye ukubwa wa tani elfu moja na kila moja imejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 5.5.

Aidha, Mhandisi Nditiye amemuomba Mhandisi Khalid Songoro wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Boatyard ambao ni wakandarasi wanaojenga meli mpya ya abiria na mizigo, kukarabati boti ya Jeshi la Polisi ya Mkoa wa Mbeya kwa gharama zao na kufanya tathmini ya gharama inayohitajika kufanyia matengenezo meli ya MV Songea iliyopo bandari ya Itungi wilayani Kyela mkoani Mbeya ili iweze kutoa huduma za usafiri.

Naye Mhandisi Songoro ameridhia ombi la Mhandisi Nditiye, na kampuni yao itakarabati boti hiyo ya Jeshi la Polisi, Mbeya pasipo wao kulipa gharama yoyote na kuwasilisha tathmini ya matengenezo ya meli nyingine na kuwasilisha Wizarani.

Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano