Baada ya msanii wa Mduara Bongo, Snura Mushi kuanika picha zikimuonesha akiwa na mpenzi wake mpya, Minihal Azad kwenye ukurasa wake wa Snapchat akimtakia siku njema ya wapendanao (Valentine’s Day)
iliyokuwa ikisherehekewa juzi Jumatano iliyopita, baadhi ya watu walibaini kuwa mpenzi huyo ni yule aliyekuwa akibanjuka na mwigizaji Salma Jabu ‘Nisha’ ambapo walimshambulia kuwa amechukua bwana wa mwenzake, Risasi Jumamosi limechimba na kubaini ukweli.

Akizungumza na gazeti hili baada ya kubanwa juu ya skendo hiyo, Snura alianika ukweli wote kwamba yeye na mwanaume huyo waliingia kwenye uhusiano wakati
tayari jamaa huyo amemwagana na Nisha na aliyewaunganisha ni Nisha mwenyewe.
Katika mahojiano hayo, Snura alifunguka kuwa, hadi anaingia kwenye mapenzi na jamaa huyo, alipitia mengi ikiwa ni pamoja na kutaka kujiua kwa sababu tu ya mapenzi.

MSIKIE SNURA
“Minihal siyo mpenzi wa Nisha wala sikumchukua kwake kwani hadi ninaingia naye kwenye uhusiano, alikuwa tayari ameshaachana naye na aliyetuunganisha ni yeye (Nisha) ambaye alimpa namba yangu ya simu,” alisema Snura.
Snura aliongeza kuwa, anawashangaa wanaodai kuwa amemchukua Minihal kwa Nisha kwani hawajui kwamba, Nisha ndiye aliyewaunganisha hadi wakawa wanafanya kazi pamoja.
Alisema kuwa, baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu ndipo walipojikuta wakiingia kwenye uhusiano wa kimapenzi.

SABABU ZA KUBANJUKA
Snura alifunguka kuwa, aliamua kubanjuka na Minihal kwa sababu alikuwa kwenye wakati mgumu wa kimapenzi baada ya kuumizwa na aliyekuwa mpenziwe ambapo mshauri mkubwa alikuwa ni jamaa huyo.
“Niliingia kwenye mapenzi na Minihal baada ya kuumizwa sana na mpenzi wangu (hakumtaja jina). Tulikuwa tukifanya kazi pamoja nikawa ninalia sana, yeye ndiye alikuwa mshkaji wangu wa karibu na mshauri wangu ndipo tukajikuta tumeingia kwenye penzi,” alisema Snura.
ALIVYONUSURUKA KUJIUA
Snura aliendelea kuweka wazi kwamba, alipitia mambo magumu mno kwenye mapenzi hadi akatamani kujiua na ndipo alipojikuta akipukutika mwili, lakini hakuna aliyemshtukia.
“Sitaki hata kukumbuka. Nilifikia hatua mbaya sana ya kutaka kujiua kwa sababu ya maumivu ya mapenzi. Ni kipindi ambacho nilipungua sana mwili, lakini watu walipokuwa wakiniuliza, niliwaambia ninafanya ‘dayati’. Ninamshukuru huyu kijana amenisahaulisha, ni mdogo, lakini anafanya mambo ambayo wakubwa hawawezi kuyafanya,” alisema Snura.

ALIVYOPOKELEWA NA WAZAZI
Baada ya kusemwa kuwa ameangukia kwa kijana mdogo na kuhojiwa iwapo wazazi wake hawatamkataa kama ilivyokuwa kwa Shilole na Nuh, Snura alisema kuwa, anashukuru kwani wazazi wa Minihal wamemkubali ingawa hajui nini kitajiri huko mbele.
“Sijui siku zijazo kitatokea nini kuhusiana na masuala ya kuanzisha familia, lakini hadi sasa ninashukuru mama yake amenikubali kwani nimeshakwenda kwao na ndugu zake pia wananikubali,” alisema Snura.
Baada ya kupambana na Snura, gazeti hili liligeukia upande wa pili wa Minihal ambaye alikiri kuwa na uhusiano na Snura na kusema kuwa alimpenda baada ya kuachana na Nisha kwa muda mrefu.
“Nilimpenda Snura baada ya kuachana na Nisha muda mrefu na aliyetuunganisha ni yeye (Nisha) ingawa hakujua kama tutakuwa na uhusiano kwani nilimuomba namba yake ya simu, akanipatia kwa ajili ya kazi,” alisema Minihal.

NENO LA MHARIRI
Tumemsiki Snura alichozungumza, lakini bado gazeti hili litafuatilia undani zaidi wa penzi hili jipya mjini kwani mastaa wengi wamekuwa wakijinadi kuwa wapenzi na wengine kudai wameoana, lakini mwisho huishia kwenye kiki za kazi zao. Kama kweli penzi hili ni la kweli na halihusiani na kiki ya muziki, tunawatakia kila la kheri!