MUNGU mkubwa! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya kusikia habari njema kuwa, mchekeshaji Bongo, Amri Athuman ‘Mzee Majuto’ au ‘King Majuto’ mwenye umri wa miaka 60 kufanyiwa upasuaji na sasa anaendelea vizuri, Ijumaa Wikienda limedokezwa.

Akizungumza na Ijumaa Wikienda akiwa katika Hospitali ya Tumaini, Upanga jijini Dar, wikiendi iliyopita, mke wa Mzee Majuto, Aisha Yusuf alisema kuwa, mumewe huyo ambaye alikuwa akisumbuliwa na saratani ya tezi dume alifanyiwa upasuaji huo Februari 12, mwaka huu na hali yake inaendelea vizuri.
“Tunamshukuru sana Mungu, Mzee Majuto anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji japokuwa tupo hospitali bado hatujajua ataruhusiwa kutoka lini ndiyo tunawasikilizia madaktari ila hana tatizo, anaendelea vizuri kabisa kwa sasa,” alisema Asha.

Kwa upande wa wasanii, Afisa Habari, Uenezi, Uhusiano na Umma wa Chama cha Waigizaji wa Kinondoni, Dar, Masoud Kaftany alithibitisha kwamba hali ya mzee huyo inaendelea vyema hivyo kuwataka wasanii kwenda kumjulia hali.
“Mzee Majuto ameshafanyiwa upasuaji na sasa ni ruksa kwa wasanii wenzake kwenda kumuona na kumjulia hali kwa utaratibu watakaoukuta kwa wauguzi, tunamshukuru sana Mungu kwa hili,” alisema Kaftany.

Mzee Majuto aliyezaliwa mwaka 1958 alianza kusumbuliwa na ugonjwa ambao hakugundulika mapema kabla ya kubainika kuwa na saratani ya tezi kisha kufanyiwa upasuaji. Ijumaa Wikienda linamuombea Mzee Majuto apone mapema