Serikali imewataka Wakuu wa Mikoa Kushiriki Kikamilifu katika kipindi cha TUNATEKELEZA ili kueleza kwa wananchi namna walivyo simamia utekelezaji wa miradi ya Maendeleo, mapambano dhidi ya rushwa na masuala yote yanayogusa ustawi wa wananchi.

Akizungumza katika Kipindi maalum cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa za miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao kwa maslahi ya wananchi.

“Kwasasa Serikali inatekeleza miradi mingi ya maendeleo, tunajenga vyumba vipya vya madarasa ili kuendana na kasi ya udahili wa wanafunzi kufuatia mpango wa elimu bure, tunajenga vituo vya afya vitakavyoongeza wigo katika utoaji wa huduma za afya, tunajenga barabara katika halmashauri zetu zote ili kurahisisha usafirishaji, haya yote yanatakiwa yasemewe na wananchi wayajue”- Alisisitiza Jafo

Aidha, Waziri Jafo aliwataka Maafisa Habari katika Serikali za Mitaa kufanya kazi kwa bidii kwa kutimiza majukumu yao kwa kuzijua Halmashauri zao vizuri, na kuacha kusubiri kuelekezwa namna ya kutekeleza majukumu yake kwani kwasasa Ofisi yake haitamvumilia Afisa Habari katika Mkoa au Halmashauri yoyote hapa nchini ambaye hatimizi wajibu wake kikamilifu.

Akifafanua Mhe. Jafo amesema kuwa Ofisi yake imekuwa ikitoa miongozo kwa watendaji wa Serikali ikiwamo Wakuu wa Mikoa juu ya namna ya kushughulikia mambo mbalimbali katika jamii, hasa mambo yanayogusa maendeleo ya wananchi.

Aliongeza kuwa Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau katika kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundo mbinu ya Elimu na maelekezo kwa wakuu wa mikoa yameshatolewa ili waweze kujielekeza katika kuongeza vyumba vya madarasa kwa sababu ya idadi kubwa ya wanafunzi wanaodahiliwa kwa sasa.

Akizungumzia mpango wa ujenzi wa Viwanda ya 100 katika kila Mkoa, Mhe. Jafo amesema baadhi ya Mikoa imefanikiwa kuanzisha viwanda zaidi ya 100 na mikoa mingine ipo katika kasi ya utekelezaji wa agizo hilo katika maeneo yao na vingi kati ya hivyo ni Viwanda Vidogo.

Kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na TBC na Kuratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO katika Awamu hii inawashirikisha Wakuu wa Mikoa, ambapo Waziri Jafo ameshiriki katika kipindi hicho kwa kutoa tathmini ya utendaji kazi wa Wakuu wa Mikoa.