Michuano ya Kombe la Shirikisho nchini (Azam Sports Federation Cup) katika raundi ya 4, inatarajiwa kutimua vumbi tena kuanzia leo Jumatano, February 21 2018.

Mechi itakayochezwa leo ni Njombe Mji itakayokuwa mwenyeji dhidi ya Mbao FC, mchezo utapigwa katika Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.

Hatua hiyo ya nne itaendelea tena siku ya Ijumaa ya tarehe 24 February kwa mechi mbili kuchezwa, ambapo Singida United itawakaribisha Polisi Tanzania, mechi ikichezwa kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

Vilevile KMC FC itacheza dhidi ya Azam FC majira ya saa moja jioni katika Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Aidha Jumamosi ya 25 February, Buselesele FC ya jijini Mwanza itachuana na Mtibwa Sugar FC kwenye Uwanja wa Nyamagana, huku Majimaji FC itacheza dhidi ya Young Africans mjini Songea.

Jumamosi hiyohiyo, Ndanda FC itacheza na JKT Tanzania katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Hatua hii ya Kombe la FA katika raundi ya 4 itakamilika 26 February kwa mechi mbili, ambapo Kiluvya United itapambana na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mabatini, huku Stand United ikisafiri mpaka Dodoma kucheza na Dodoma FC.