Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Faustine Ndugulile baada ya kuwasili kwenye Kituo cha Afya cha Karume katika Kata ya Bugogwa wilayani Ilemela kuweka jiwe la Msingi la kituo hicho, Februari 20, 2018. Alikuwa katika ziara ya mkoa wa Mwanza.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabulla wakati alipowasili kwenye Kituo cha Afya cha Karume katika Kata ya Igogwa wilayani Ilemela Februari 20, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wakati alipokagua Kituo cha Afya cha Karume katika Kata ya Igogwa wilayani Ilemela Februari 20, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wakati alipowasili kwenye uwanja wa michezo kuhutubia mkutano wa hadhara Katika Kata ya Bugogwa wilayani Ilemela Februari 20, 2018.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Igogwa wilayani Ilemela wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowahutubia karibu na Kituo cha Afya cha Karume, Februari 20, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa michezo uliopo karibu na Kituo cha Afya cha kata ya Igogwa wilayani Ilemela

SERIKALI imepeleka sh. bilioni 2.6 katika Jiji la Mwanza kwa ajili ya kugharamia uboreshaji wa vituo vya afya ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Hayo yalibainika jana (Jumanne, Februari 20, 2018) wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokagua na kuweka jiwe la msingi la kituo cha afya cha Karume.

Waziri Mkuu alikagua ukarabati wa kituo hicho kilichopo kwenye kata ya Bugogwa wilayani Ilemela akiwa katika siku ya sita ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

Alisema uboreshaji huo ulihusisha ujenzi wa chumba cha upasuaji, maabara, chumba cha kujifungulia, jengo la mama na mtoto na wodi ya wanawake na wanaume.

Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na uboreshaji wa kituo hicho, ambapo Serikali inatarajia kupeleka sh. milioni 200 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha inasogeza huduma za afya karibu na wananchi. Uboreshaji wa kituo cha afya cha Karume umegharimu takriban sh. milioni 497 hadi hivi sasa.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa mkakati wa Rais Dkt. John Magufuli ni kuimarisha sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu karibu na maeneo yao ya makazi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndungulile alisema Serikali imetoa sh. bilioni 2.6 kwa ajili ya uboreshaji wa vituo vya afya jijini Mwanza.

Alisema fedha hizo zinalenga kuboresha vituo hivyo ili kuviwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi wa jiji zikiwemo huduma za afya ya mama na mtoto, upasuaji na maabara.

Awali, Waziri Mkuu alifungua zahanati ya Bulale iliyopo katika kata ya Buhongwa wilayani Nyamagana na kisha alitoa vitambulisho vya matibabu kwa wazee 250. Jumla ya wazee 5,398 wilayani humo wamepatiwa vitambulisho vya matibabu.