Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa amezindua Kliniki ya Methadone katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure kwa ajili ya kusaidia waathirika wa dawa za kulevya.
Uzinduzi huo umefanyika Februari 20,2018 katika hospitali ya Sekou Toure na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali likiwemo Shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI), ICAP na wafadhili ambao ni wa Watu wa Marekani kupitia Centres for Disease Control and Prevention (CDC).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pia alizindua muongozo wa uendeshaji wa nyumba za waathirika wa dawa za kulevya (Soba Houses) ambao unalenga kuwawezesha wamiliki wa nyumba hizo kuziendesha vizuri na kuwasaidia ipasavyo.
Waziri Mkuu aliwatahadharisha watanzania wasijishughulishe kuzalisha,kusambaza,kuuza na kutotumia dawa za kulevya kwani Serikali imejizatiti katika vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya.
“Leo hii mmeona na tumeshuhudia ushuhuda wa vijana walioathirika na dawa za kulevya walikuwa wanaleta athari katika jamii,walikuwa wanaleta vurugu,wanakaba lakini baada ya kufika katika kliniki hali zao zimekuwa nzuri,nataka wanaouza dawa hizo waache na watumiaji wafike hospitali”,alisema Waziri Mkuu.
“Serikali tuna wadau wanaotuunga mkono kuna AGPAHI, ICAP, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wanatufanya tufike hapa tulipo,niwasihi watanzania popote mtakapoona vijana wetu wameathirika na dawa waleteni kliniki wasajiliwe,wapewe dawa na niiombe jamii iwaamini hawa waliobadilika kwani wamejua athari za dawa za kulevya”,aliongeza Waziri Mkuu.

Aidha alisema hivi sasa serikali inaendelea kutafuta maeneo kwa ajili ya shughuli za ujasiriamali ili watu watakaotaka kujifunza ujasiriamali watumie maeneo hayo kwa ajili ya kuokoa vijana.
Naye Mwakilishi wa Ubalozi wa Marekani, Dk. Maestro Evans ambao wamesaidia kuanzishwa kwa kliniki hiyo kupitia shirika la AGPAHI na ICAP kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia CDC alisema kliniki hiyo itasaidia kupunguza athari zinazotokana na dawa za kulevya kama vile maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Dk. Evans aliishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendelea kutambua mchango wa serikali ya Marekani katika kuwahudumia wananchi katika masuala ya afya ikiwemo VVU na Ukimwi, Malaria na huduma za mama na mtoto.
Aidha alisema serikali ya Marekani itaendelea kusaidia kazi zinazofanyika katika eneo la kushughulikia dawa za kulevya na kupunguza athari zinazotokana na dawa za kulevya na kusaidia waathirika.
Akizungumza wakati uzinduzi huo Mganga Mkuu wa mkoa wa Mwanza Dk. Leonard Subi alisema kituo hicho kimetokana na mchango mkubwa wa wadau wakiwemo AGPAHI, ICAP kwa msaada wa watu wa Marekani.
Alisema lengo la kuanzishwa kwa kituo hicho ni kuwasaidia watu walioathirika na dawa za kulevya ili kukabiliana na madhara yatokanayo na dawa hizo ikiwemo homa ya ini na maambukizi ya VVU.
“Wadau wetu ICAP na AGPAHI kwa ufadhili wa Watu wa Marekani wamesaidia fedha kwa ajili ya dawa na samani za ndani ya kliniki hii”,alisema.
Nao waathirika wa dawa za kulevya,Abdallah Abdul na Nyamizi Sospeter waliishukuru serikali kwa kuwaondoa katika wimbi hilo la dawa za kulevya na kuahidi kuwa watu wazuri kwa kutofanya vitendo vya uhalifu mtaani.
Aidha waliiomba serikali kuwasaidia kwa kuwapa elimu ya ujasiriamali ili waweze kupata ujuzi utakaowawezesha kufanya kazi na kupata kipato kitakachowasaidia kujiinua kiuchumi kwani hawakuwa na kazi za kufanya zaidi ya kukaba watu mtaani.
Kamishna mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA),Rogers Siyanga alisema kliniki hiyo iliyozinduliwa italeta nafuu kubwa kwa waathirika wa dawa za kulevya lakini pia kupunguza madhara ya arosto na madhara yatokanayo na dawa hizo mfano Ukimwi,homa ya ini,magonjwa ya ngozi na magonjwa ya meno.

Alisema serikali itawapatia vitambulisho waathirika wa dawa za kulevya walioanza kupata matibabu ili kuwaepusha na usumbufu unaoweza kujitokeza mtaani kwa baadhi ya watu kutoamini kama waathirika wa dawa hizo wamebadilika tabia baada ya kuanza kuhudhuria kliniki.
“Vyombo vya dola vitakapokutana na watu hawa,naomba tusiishi kwa historia,wakikuonesha kitambulisho kwamba anahudhuria hospitali kupata dawa naomba umpeleke hospitali usiendelee kumwadhibu”,alisema Siyanga.
Siyanga alitoa wito kwa watu walioathirika na dawa hizo wajitokeze kupata matibabu ili wawape nafuu na familia za watu waliothirika na dawa za kulevya wawapeleke ndugu zao wakapate dawa katika Kliniki ya Methadone iliyopo katika hopitali ya Sekou Toure.