Rais wa Fifa, Gianni Infantino anaongoza kikao cha siku moja kujadili masuala mbalimbali kuhusu soka la vijana na wanawake na maendeleo ya mchezo wake kwa jumla.

Mara baada ya kuwasili ukumbi hapo akiwa katika msafara wa magari manne, Infantino aliyefuatana na Rais wa CAF, Ahmad Ahmad pamoja na Rais wa TFF, Wallance Karia, Mjumbe wa CAF na mwenyekiti wa BMT, Leodegar Tenga na Kaimu Katibu wa TFF, Wilfred Kidau alivalishwa mgolole na wamasai waliokuwa akicheza ngoma nje ya ukumbi wa Mwalimu  Nyerere.

Rais huyo wa FIFA baada ya kuvalishwa mgolole pamoja na Rais wa CAF, alivalishwa bangili na alipewa kirungu kiilichotengenezwa kwa kisu.

Walipoingia ndani ya jingo hilo, walipata zawadi maalumu kutoka Bodi ya Utalii Tanzania pamoja na nakala zinazozungumzia Tanzania na hifadhi zake.

Awali wajumbe kutoka nchi 19 walitangulia wakiongozwa na Katibu mkuu wa Fifa, Fatma Samoura ambaye naye alionekana kufurahia mapambo ya kimasai kwa wamasai waliokuwa wakiuza bidhaa zao.