Leo February 23, 2018 Watu watano akiwemo Ofisa wa Benki ya NBC Makao Makuu wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya Mwanaharakati wa Ujangili, Wayne Lotter.

Akiwasomea mashtaka yao Wakili wa serikali Mwandamizi, Yamiko Mlekano amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa washtakiwa wanakabiliwa na makosa mawili.

Alidai kuwa washtakiwa ni Nduimana Jonas (40) ‘Mchungaji’ ambaye ni raia wa Burundi, Godfrey Peter (42) mfanyabiashara, Innocent Pius (23) mfanyabiashara, Chambie Juma (32) mfanyabiashara na Robert Harride (31) Ofisa wa Benki ya NBC.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa la kula njama ya kufanya mauaji ya Mwanaharakati wa kupinga Ujangili, Wayne Lotter katika tarehe tofauti kati ya July 1,2017 na August 16,2017.

Katika kosa la pili washtakiwa hao wanadaiwa kuwa, katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selasie Kinondoni DSM August 16, 2017 walimuua Mkurugenzi na Mwanzilishi-Mwenza wa Shirika lisilo la kiserikali la PALMS Foundation, Wayne Lotter (52).

Baada ya kusomewa mashtaka hayo hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.

Wakili Mlekano alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi March 6,2018 kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa hao wataunganishwa na mfanyabiashara Rahma Almas ‘baby'( 37 ), Mohammed Maganga (61) ambaye ni mchimba makaburi na Khalid Almas (33).