Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akimkaribisha ofisini mgeni wake, Balozi wa Uholanzi nchini, Jeroen Verheul mara baada ya kuwasili.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa Uholanzi nchini, Jeroen Verheul.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe amekutana na Balozi wa Uholanzi nchini, Jeroen Verheul na kufanya nae mazungumzo kuhusu mpango wa kukamilisha mradi wa maji wa kitaifa wa Handeni (HTM) uliopo katika wilaya za Handeni na Korogwe, mkoani Tanga.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye ofisi za wizara za Ubungo Maji, Jijini Dar es Salaam, yalilenga katika kutatua changamoto za mradi huo ili uweze kukamilika na kutoa huduma kwa ufanisi kwa wakazi ambao kwa sasa wamefikia 300,000 kulinganisha na 180,000 kama lengo la awali katika vijiji 79 vya wilaya za Handeni na Korogwe.

Katika kikao hicho Waziri Kamwelwe na Balozi Verheul walikubaliana hatua za haraka zichukuliwe kwa lengo la kuondoa vikwazo vyote na kutekeleza mpango huo mara moja.