Pacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti wamesema wakati wowote wataenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi juu ya afya zao.

Pacha hao wanaosoma Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (Rucu), wanaendelea kupatiwa matibabu ya moyo kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Maria na Consolata walifikishwa JKCI wakitokea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, walikokuwa wamelazwa tangu Desemba 28, 2017.

Katika ujumbe wao walioutuma jana jioni Februari 23, 2018, pacha hao wamesema wanahitaji maombi zaidi wakati huu wanapotarajia kufanyiwa uchunguzi nchini Afrika Kusini.

“Jamani ni sisi Maria na Consolata tunaomba sala zenu maana tunatarajia kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi zaidi ila kwa sasa tuko Dar es Salaam. Tarehe tutajuzana. Tunahitaji sala zenu,” waliandika.

Maria na Consolata hutumia simu moja katika mawasiliano.