MWANAMUZIKI wa Bongo Fleva, Khadija Shabani ‘Keisha’ ameeleza sababu iliyomfanya akae kimya kwa muda mrefu.

Keisha ambaye amewahi kutamba na nyimbo kadhaa ikiwemo Uvumilivu, Usinitenge, Nimechoka aliyomshirikisha Nasibu Abdul ‘Diamond’ amekuwa kimya kwa muda mrefu kiasi cha kuwafanya mashabiki wajiulize amepotelea wapi.

Keisha alisema kuwa, moja ya sababu ya yeye kukaa kimya kwa muda mrefu ni kutokana na majukumu kumzonga
kama kulea na masomo, lakini kwa sasa yupo freshi na mashabiki wake wajiandae kupokea kazi zake.

“Nilikuwa kimya kwa muda kutokana na majukumu ya kifamilia niliyokuwa nayo ya kulea, kusoma na mambo mengine na ndiyo maana nilikuwa sisikiki na wala siyo kwamba mume wangu amenizuia nisiimbe.
“Kwa sasa natarajia kutoa kibao kipya ambacho kitatoka hivi karibuni na tayari nimesharekodi ambapo sijamshirikisha mtu. Kuna majina matatu ambayo nimeyapendekeza kuupa jina wimbo huo hivyo nitaliweka wazi hapo baadaye,” alisema Keisha.