Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, imekamata mifuko 15 ya sukari ya magendo inayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh1 milioni.

Sukari hiyo imekamatwa leo Ijumaa Februari 23, 2018 na kuthibitishwa na kaimu mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Godwin Gondwe.

Gondwe amesema kukamatwa kwa sukari hiyo mifuko 15 sawa na kilo 750 ni mwendelezo wa operesheni walioanzisha kwa ajili ya kufuatilia na kuwadhibiti wafanyabiashara wanaokwepa kodi na kuisababishia Serikali hasara.

Amewataka wafanyabiashara kufuate taratibu katika kufanyabiashara zao kwa kulipa kodi, waache tabia ya kufanya magendo kwani Serikali ipo macho na haiwezi kukubali hasara.

“Hili ni onyo kwa wafanyabiashara wote ambao wanafanya biashara za magendo, kamwe hatuwezi kuwaacha wala kuwasamehe kama watafanya magendo. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vipo na tutawakamata,” amesema Gondwe.

Naye meneja wa TRA Wilaya ya Korogwe, Remigius Lwambano amesema mifuko hiyo 15 thamani yake ni Sh1.6 milioni kwa bei ya sasa ya mfuko wa kilo 50 kwa Sh110,000.

Amesema sukari hiyo inaonyesha inatoka nchini Brazil, imeingia nchini kupitia njia za panya na kusambazwa kwa wananchi.