Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Bibi. Consolata Mushi (kushoto) akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya BAKITA pamoja na uzinduzi wa kanzi data ya wataalamu wa Kiswahili jana Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe na kulia ni Katibu Mkuu Wizara hiyo Bibi. Suzan Mlawi.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi. Suzan Mlawi akizungumza na wajumbe wa bodi mpya ya BAKITA (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo pamoja na uzinduzi wa kanzi data ya wataalamu wa Kiswahili jana Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na wajumbe wa bodi mpya ya BAKITA (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo pamoja na uzinduzi wa kanzi data ya wataalamu wa Kiswahili jana Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) akimpa mkono wa pongezi Mwenyekiti wa bodi mpya ya BAKITA Dkt. Methord Samwel (kulia) baada ya kuzindua bodi hiyo pamoja na kufanya uzinduzi wa kanzi data ya wataalamu wa Kiswahili jana Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi. Suzan Mlawi.

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (wapili kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kanzi data ya wataalamu wa Kiswahili wakati wa uzinduzi wa bodi ya BAKITA pamoja na uzinduzi wa kanzi data ya wataalamu wa Kiswahili jana Jijini Dar es Salaam. Wapili kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi. Suzan Mlawi na kushoto ni Mwenyekiti wa bodi mpya ya BAKITA Dkt. Methord Samwel.

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) akimkabidhi zawadi mwenyekiti mstaafu wa bodi ya BAKITA Prof. Martha Qorro (kulia) wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya BAKITA pamoja na uzinduzi wa kanzi data ya wataalamu wa Kiswahili jana Jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kiswahili ya taifa (BAKITA) Dkt. Methord Samwel akizungumza baada ya bodi yake kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo jana Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (wapili kushoto) katika picha ya pamoja na wajumbe wa bodi mpya ya BAKITA baada ya kuzindua bodi hiyo jana Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Katibu Mkuu wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi. Suzan Mlawi na kushoto ni mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili la Taifa Dkt. Methord Samwel.

Watanzania wametakiwa kuchangamkia fursa za utafiti, fursa za ushirikiano wa kitaalamu na fursa za ajira katika kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ili nafasi zinapotangazwa watanzania wenye sifa wajitokeze kwa wingi kupigania nafasi hizo kufundisha lugha ya Kiswahili katika nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) pamoja na uzinduzi wa kanzi data ya wataalamu wa Kiswahili jana Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Mwakyembe amesema kuwa leo hii kiswahili kimetandawaa na kuenea kote duniani huku kikipewa kipaumbele katika nyanja mbalimbali ikiwemo hapa nchini na hata nchi za nje, kwani nchi mbalimbali zimekua zikionyesha mahitaji ya wataalamu wa lugha ya Kiswahili hivyo kuwataka watanzania kuwa sehemu ya mahitaji hayo.

Aidha Mhe. Mwakyembe ameiambia Bodi mpya ya BAKITA kuwa Wizara inaitarajia bodi hiyo kuwa muhimili wa BAKITA na chachu ya kuirejeshea nchi ukombozi na ukuzaji wa lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania kwa kufanya kazi kisayansi zaidi kuliko kutumia nguvu na rasilimali nyingi bila tija.

“Leo tunazindua rasmi bodi ya BAKITA, naamini kuwa mko tayari kufanya kazi hii kwa juhudi, uteuzi wenu umezingatia sana masharti na weledi kwa mujibu wa sheria ya BAKITA kwani hakuna hata mmoja wenu aliyeteuliwa kwa kubahatisha” amesema Mhe. Mwakyembe.

Akizungumzia kuhusu kanzi data ya wataalamu wa lugha ya Kiswahili nchini Waziri Mwakyembe amesema kuwa kanzi data hiyo itasaidia kuwapata na kuwajua wataalamu wa Kiswahili tulionao nchini kwa ajili ya mahitaji ya ndani na nje ya nchi lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa watanzania wenye sifa sahihi wanapata nafasi za kazi na kueneza lugha ya Kiswahili duniani hivyo ni wajibu wa Baraza la Kiswahili la Taifa kuboresha kanzi data hiyo ili ikidhi mahitaji ya soko la ajira la wataalamu wa lugha ya Kiswahili.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi. Suzan Mlawi amesema kuwa wazo la kuwa na kanzi data ya wataalamu wa lugha ya Kiswahili ni jambo kubwa sana na kwa kuwa kanzi data itatumia njia ya Tehama wananchi watahudumiwa kwa haraka kwa wepesi na kwa usahihi.