Rais Magufuli amesema anasubiri ripoti ya Wizara ya Ardhi kuhusu wananchi waliovamia uwanja wa ndege wa Mwanza lakini amebainisha kuwa serikali haiwezi kukimbilia kuondoa kaya zaidi ya 1,900 zinazodaiwa kuvamia eneo hilo na badala yake itaangalia njia bora ya kufanya.

Rais Magufuli amesema hayo aliporejea nchini akitokea Uganda ambako amehudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliomalizika jana Mjini Kampala.
Hata hivyo Rais Magufuli amewataka wananchi waliopo katika eneo hilo wasiendeleze makazi yao wakati uamuzi wa serikali unasubiriwa.
“Bahati nzuri naibu Waziri wa Ardhi yupo hapa, kafanyieni kazi changamoto hii na mnipe ripoti,” amesema Rais Magufuli.
Baada ya kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza Rais Magufuli ameelekea nyumbani kwake Chato Mkoani Geita kwa mapumiziko.