WAZIRI Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania(CKHT) Mizengo Pinda ametoa wito kwa Wataalamu wa Chuo hicho kutoa mafunzo ambayo yatawasaidia wananchi kuleta mageuzi ambayo yatawezesha katika ujenzi wa Tanzania ya Viwanda na hivyo kutimiza lengo la Serikali ya Awamu ya Tano.

Mkuu huyo wa Chuo Kikuu hicho alitoa kauli hiyo mjini hapa wakati akizungumza na Watumishi na Wanachuo wa CKHT Tawi la Tabora wakati wa ziara ya siku moja chuoni hapo.

Alisema kuwa Chuo hicho kinayo nafasi kubwa ya kuleta mageuzi yatakawawezesha wananchi wengi waweze kutoa mchango wao katika ujenzi wa uchumi wa viwanda hapa nchini na hivyo kusaidia katika mapambana dhidi ya umaskini.

Mkuu huyo wa Chuo hicho alisema kuwa hiyo itawezekana ikiwa elimu itakayotolewa itakuwa ikisaidia katika kujibu matatizo ya wananchi kwa kuwa na wahitimu ambao wanaweze kuwa mfano kwa wananchi ili waweze kujifunza kwao mbinu zitakazowawezesha kujiletea maendeleo.

Aidha Waziri Mkuu huyo Mstaafu aliwataka Watendaji na wadau mbalimbali kusaidia kuwahamasisha walimu wengi hasa wa shule za Msingi kujiunga na Chuo hicho katika maeneo mbalimbali ili waweze kujiendeleza zaidi na kuboresha mbinu za ufundishaji.

Alisema kuwa Chuo Kikuu Huria kikitumiwa vizuri kinamchango mkubwa wa kuleta mageuzi katika sekta ya elimu na nyingine na kuweza kuboresha ufaulu hata katika maeneo ambayo wanafunzi walikuwa hawafanyi vizuri katika mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi.

Waziri Mkuu huyo Mstaafu aliongeza kuwa hatua itasaidia sana kuleta tija katika mbinu ufundishaji itakayoasaidia katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi wote hata wale wenye mahitaji maalumu.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania amewaagiza Wataalamu wake kuangalia jinsi ya kuandaa utaratibu na vigezo vya upimaji wa vituo mbalimbali katika matawi yake nchini ili kuona ni Kituo gani kimefanya vizuri na Kituo cha mwisho.

Alisema kuwa hatua hiyo itawasaidia kujua kama Kituo kimekuwa cha mwisho sababu ni nini na kama ni walimu waweze kutatua na hivyo kufanya waweze nao kufanya vizuri.

“Kama tunavyofanya katika elimu ya msingi na sekondari , nimeagiza Wataalamu waangalie jinsi ya kuanza kupima ufaulu wanachuo wetu katika Vituo vya Chuo Kikuu Huria ili tujue cha kwanza na cha mwisho…kama kituo kitakuwa cha mwisho tujue na sababu, kama ni udhaifu wa wakufunzi tuweze kulifanyia kazi” alisema Mkuu huyo wa Chuo.

Naye Mkurugenzi wa CKHT Tabora Noel Nkombe alisema kuwa Tawi hilo linakabiliwa na tatizo na ukosefu wa majengo kwa ajili ya utoaji wa huduma kwa wanachuo , jambo ambalo limewafanya wafanye kazi kwa kuhama hama mara kwa mara.

Alisema kuwa ili kukabiliana na tatizo hilo tayari wamepata kiwanja katika eneo la Ipuli katika Manispaa ya Tabora ambapo katikati ya mwezi ujao wanatarajia kuendesha harambee kwa ajili ya kupata fedha za kuanza ujenzi wa awali.

Akisoma risala ya wanachuo Katibu wa Serikali ya Wanachuo Tawi la Tabora Husna Suleyman alisema kuwa kwa kutambua tatizo la majengo kwa ajili ya Kituo chao , wao kwa hiari hayo wameamua kuchanga kila mmoja shilingi 30,000 ambapo zimepatikana milioni 6.1.

Alisema kuwa hatua hii inalenga kuunga mkono juhudi za uongozi wa CKHT za kutaka kuboresha mazingira ya wao kujisomea.A