Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma amewaagiza Mahakimu wote nchini kutoa bure nakala za hukumu kwa wananchi ili kurahisisha upatikanaji wa Haki.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika Mahakama za wilaya ya Uvinza na Kasulu mkoani Kigoma leo, Jaji Mkuu amewaambia Mahakimu hao kuwa endapo watakutana na kikwazo cha Sheria, au Kanuni katika kutekeleza agizo hilo wasisiste kumpelekea mapendezo yao.

Jaji Mkuu amefikia uamuzi huo kutokana na Maboresho ya Huduma za Mahakama yanayoendelea pamoja na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania (2015/16 hadi 2019/20).

Alisema ni haki ya kila Mwananchi aliyekuwa na kesi mahakamani kupatiwa nakala ya hukumu yake ndani ya siku 21 tangu kusomwa kwa hukumu hiyo au mapema iwezekanavyo mara baada ya kesi yake kutolewa hukumu. Nakala ya hukumu imekuwa ikilipiwa kiasi cha shilingi elfu kumi (10,000) kama gharama ya uandaaji wa nakala hiyo.

Akizungumzia maboresho ya huduma za mahakama, Prof. Juma alisema Mahakama inao mpango wa kuanzisha Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) ili kutatua changamoto ya upungufu wa Mahakama kwenye baadhi ya Maeneo nchini ikiwemo mikoa ya Tabora na Kigoma. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Zaidi ya watanzania milioni 25 wako mbali na huduma za Mahakama.

Alisema wananchi wa Wilaya ya Kasulu hulazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 376 kufuata huduma za Mahakama Kuu katika mji wa Tabora na kuongeza kuwa hivi sasa Mahakama imeshaanza ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu kanda ya Kigoma unaotarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu. Aliongeza kuwa Mpango Mkakati wa Miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania unaainisha namna ya kutatua changamoto mbalimbali za Mahakama ikiwemo ya umbali wa Mahakama na wananchi.

Akizungumza na watumishi wa Mahakama, Jaji Mkuu aliwataka watumishi hao kuzingatia maadili ya kazi na Mahakamas zisiwe sehemu ya rushwa ili kujenga taswira nzuri ya Mhimili huo kwa wananchi.

Alisema Mahakama haina budi kushirikiana na wadau na ushirikiano huo uwe ni ule usioingilia mamlaka ya mwenzake bali kila mhimili usimamie mipaka yake.

“Heshima ya Mahakama itaongezeka tu kama watumishi watakuwa na maadili mema ikiwa ni pamoja na kauli nzuri kwa wananchi wanaofika Mahakamani kutafuta haki zao”,alisema Jaji Mkuu.

Awali, Mkuu wa wilaya ya Uvinza, Mwamvua Mrindoko alimweleza Jaji Mkuu changamoto zinazoikabili wilaya yake kuwa ni pamoja na kuwepo kwa makossa makubwa ya kiuhalifu kutokana na madhara ya wakimbizi yakiwemo mauaji, ungang’anyi wa kutumia silaha, pamoja na ubakaji.

Alizitaja changamoto nyingine kuwa ni kukosekana kwa gereza katika wilaya yake na kuiomba Mahakama ya Tanzania kujenga jengo lake la Mahakama ya wilaya ili kurahisisha suala zima la upatikanaji wa haki kwa wamanchi.

Jaji Mkuu anaendelea na ziara yake ya kukagua shughuli za Mahakama katika kanda ya Tabora ambapo leo ametembelea Mahakama za Wilaya za Kasulu na Uvinza .