Madaktari Bingwa wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na Madaktari wa Hosipitali ya BLK India leo wamefanya upasuaji maalum wa mgongo kwa kutumia matundu (Minimal Invasive Spine Surgery) kwa mgonjwa aliyedhoofika uti wa mgongo.

Kwa Mujibu wa Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo na Taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam, Upasuaji huo umefanywa kwa mafanikio makubwa ukiwashirikisha Madakatari Bingwa wanne wakiongozwa na Profesa Joseph Kahamba wa MOI na Dkt. Puneet Girdhan kutoka hosipitali ya BLK.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa upasuaji huo umefanyika kwa mafanikio makubwa kwa muda wa masaa manne ambapo pamoja na upasuaji huo, MOI imeanzisha huduma za upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu ( Athroscopy ).

“ Tayari wagonjwa 300 wameshafanyiwa upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu kwa ufanisi mkubwa na wagonjwa wengine wameendelea kunufaika na huduma hii” Inasisitiza sehemu ya Taarifa hiyo

Kutokana na mabadiliko ya teknolojia ya matibabu, upasuaji wa kupanua njia za mishipa ya fahamu na kuimarisha uti wa mgongo kwa nyenzo za kisasa umeshika hatamu na Taasisi hiyo imeendelea kufanya mabadiliko ili kuendana na hali hiyo.

Taasisi ya MOI na Hospitali ya BLK ya India zilianzisha ushirikiano mwaka 2016 na hii ni mara ya pili kwa wataalamu kutoka hosipitali hizi kufanya upasuaji kwa kushirikiana.