Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mtwara, Stephen Mafipa kumtafuta popote alipo na kumkamata aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi, Fortunatus Kagoro kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha.

Mbali na Kagoro pia kaimu mweka hazina, Heri Hamad, ofisa mipango, Teresia Nsumba nao ameagiza wakamatwe na baada ya uchunguzi watakaobainika kwamba hawajahusika na ubadhilifu huo watarudishwa kazini, “Lazima fedha za Serikali zitumike kama ilivyokusudiwa.”

Taarifa iliyotolewa leo Februari 26, 2018 na ofisi ya Waziri Mkuu inaeleza kuwa watendaji hao wanadaiwa kutumia Sh1.8bilioni zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la halmashauri ya mji wa Masasi kwa kuchora mchoro na kujenga msingi katika maeneo mawili tofauti.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri ya mji wa Masasi na halmashauri ya wilaya ya Masasi akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara.

Amesema mwaka 2014 Serikali ilipeleka Sh575milioni wilayani Masasi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la halmashauri hiyo na fedha hizo ziliishia kutumika katika hatua za maandalizi ya awali ikiwa ni pamoja na kutengeneza michoro ya jengo.

Amesema 2016/2017 Serikali ilipeleka tena Sh1.25 bilioni kwa ajili ya ujenzi huo, ambapo halmashauri hiyo ilienda kutafuta eneo lingine na kufanya tena shughuli zilizokuwa zimefanyika na kuanza ujenzi ambao umeishia katika msingi na fedha zimeisha.

Pia amewataka watendaji hao kutotumia fedha za makusanyo ya ndani kwa ajili ya kuziba pengo la fedha za mradi huo ambazo baadhi yake hazijulikani zilipo na amewaagiza madiwani kutoruhusu jambo hilo.