Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akifungua Kikao kazi cha kujadili mpango wa utekelezaji wa miradi ya inayotekelezwa kwa Fedha za mfuko wa Maendeleo ya Serikali za Mitaa.

Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe akizungumza na wajumbe wa Kikao Kazi(hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua Kikao hicho.

Katibu Mkuu OR-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Dkt.Laurean Ndumbaro akizungumza na wajumbe wa Kikao Kazi cha kujadili mpango wa Utekelezajo wa Miradi ya LGDG.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo (Mbele aliyesimama) akizungumza na wajumbe wa Kikao kazi cha kujadili mpango wa utekelezaji wa miradi ya LDGD.

Baadhi ya Wakurugenzi wa OR-TAMISEMI wakibadilishana mawazo wakati wa Kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa Miradi ya LGDG.

Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Wakili Kiomoni Kiburwa Kibamba akiwa na Mchumi wa Jiji wakifuatilia Kikao kazi cha kujadili Utekelezaji wa Miradi ya LGDG kilichofanyika Chuo cha Mipango Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amewataka viongozi wa Halmashauri zote Nchini kupitia mipango iliyopo (Review) na kupanga Upya Kimakati miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa kwa Fedha za mfuko wa Maendeleo ya Serikali Mitaa (LGDG).

Waziri Jafo ameyasema hayo kwenye Kikao Kazi cha kujadili Mpango wa Utekelezaji wa Miradi ya LGDG iliyoboreshwa kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 kilichohusisha baadhi ya Wah. Wabunge, Mameya, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na Maafisa Mipango kilichofanyika katika chuo cha Mipango kilichopo mjini Dodoma.

Waziri Jafo alisema kuwa Bajeti ya Mfuko wa Maendeleo ya Serikali za Mitaa kwa mwaka huu wa Fedha ni Bil.251 ambazo hugawanywa kwa halmashauri zote Nchini. Fedha hizi ni nyingi sana na zinatosha kutekeleza miradi michache yenye Tija na itakayopunguza changamoto kwa wananchi wetu lakini kinachofanyika ni kuwa halmashauri hugawanya kiasi wanachopata kwenye miradi mingi ambapo sio rahisi kuona matokeo kwakuwa miradi mingi haikamiliki.

“Katika Halmashauri nyingi badala ya kugawanya Fedha hizi za Ruzuku kwenye miradi mingi kwa viwango kidogo kidogo ni vyema sasa tukajieleza kwenye miradi michahe ambayo tutahakikisha inakamilika kwa mwaka wa Fedha husika na kuanza kutoa huduma kwa jamii” Alisema Jafo.

“Kuna miradi viporo mingi sana katika Halmashauri zetu ukiangalia Sekta ya Afya utakutana Maboma mengi ambayo yangekamilika yangetumika kama Zahanati au Vituo vya Afya, Elimu utashuhudia magofu ya kutosha ambayo yangekamilika yangetumika kama vyumba vya madarasa hii yote ni kutokana na kupanga miradi mingi kwa wakati mmoja sasa kwa mwaka huu na kupitia Kikao hiki mfanye mapitio Upya na mpange miradi michache itakayokamilika kupitia bajeti kwa mwaka huu” Aliongeza Jafo.

Waziri Jafo alisisitiza kuwa Katika Bajeti ya LGDG mwaka huu Bil.66 zimeelekezwa kwenye Sekta ya Afya nataka mkazisimaie mkakamilishe Maboma yaliyotelekezwa kwa kipindi kirefu na yakamilke tayari kwa kutoa huduma halkadhalika katika maeneo mengine yote ambayo Fedha hizi zitatumika.

Waziri Jafo alimalizia kuwa kikao hiki sio Semina wala eneo la mapumziko kwa viongozi wa halmashauri bali ni Kikao kazi hivyo Kitumike kama fursa adhimu na muhimu ya kufanya Mapitio ya Mipango ya halmashauri ambayo ikitekelezwa italeta matokeo Chanya na kuwapunguzia adha wananchi wetu.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhandishi Musa Iyombe amesema Kikao hiki ni Maalumu kwa Viongozi wote ambao wanahusika moja kwa moja na kuwaletea wananchi maendeleo ili kwa pamoja tukubaliane, tushauriane na tuelekezane namna bora ya kutekeleza miradi hiyo ambayo inaonekana eneo la Mipango halijafanyiwa kazi kikamilifu.

“Viongozi wenzangu lazima suala la mipango liangaliwe kwa Makini katika Halmashauri zetu, Jambo hili lisipofanyika kwa Umakini lina madhara makubwa kwa Jamii, litaturudisha nyuma kimaendeleo na kila siku tutaona hatufanikiwa katika miradi yetu kwa sababu tu tulikosa umakini katika kuandaa Mipango yetu, hebu tupitie upya mipango yetu na tuhakikishe tunamaliza mradi mmoja kwanza kabla ya kuanza mwingine” alisema Mhandisi Iyombe.

Akizungumza na wajumbe wa Kikao kazi Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Menejiment ya Utumishi wa umma na Utawala bora Dkt.Laurean Ndumbaro amewakumbusha watumishi wote kufanya kazi kwa kuzingatia Hotuba ya Mhe.Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alipohutubia Bunge na kusisitiza Uwajibikaji, Utumishi wa Umma unaojali misingi ya Uadilifu, Weledi wa Kitaaluma, Maadili na Uadilifu katika Utendaji kazi wetu.

“Watumishi wanapaswa kuwajibika kwa Serikali iliyopo Madarakani kwa kutekeleza yale yote yanayowapasa kutekeleza kwa mujibu wa miongozo kwa watumishi wenzetu tunaofanya nao kazi na kwa wananchi tunaowatumikia, tuwape haki yao ya msingi ya kuwahudumia na kuwalete maendeleo.” Alisema Dkt. Ndumbaro.

Kupitia Kikao hiki washiriki kutoka katika Halmashauri zote watapitia Upya miradi ya maendeleo waliyopanga kutekeleza kupitia Fedha za “LGDG” kwa kuzingatia maelekezo watakayopewa kabla ya kupokea Fedha hizo kwa ajili ya utekelezaji.