Msanii wa miondoko ya singeli Man Fongo amefunguka na kusema yupo tayari hata kupelekwa Mahakamani kujibu mashtaka ya kutumia kazi ya wanamuziki wa zamani wa ‘Kilwa Jazz Band’ kwa madai lengo la kutumia wimbo wao ni kutaka kuufikisha mbali singeli.
Man Fongo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye kipindi cha eNews kutoka EATV akiwa katika viwanja vya BASATA, Ilala Jijini Dar es Salaam baada ya wamiliki wa wimbo ambao ameuimba ‘lau nafasi’ kumfungulia mashtaka kutokana na kuimba ‘sample’ hiyo bila ya kuwa na vibali halali kutoka kwa bendi ya Kilwa Jazz

“Ni yale yale mambo yetu yaliyokuwa yakinisumbua tokea mwezi Februari kuhusiana na wimbo wangu mpya wa Lau nafasi. Kuna vikwazo vingi vimetokea nimeitwa BASATA kuja kuangalia kitu gani kinachoendelea ila hadi sasa hivi naona mambo yameshakuwa mazito kwa sababu naona kama imeshatumwa barua hapa”, amesema Man Fongo.

Pamoja na hayo, Man Fongo ameendelea kwa kusema “nipo teyari kwenda kokote kwa sababu mimi ni msanii nipo radhi kuupambania muziki wa singeli kama watanzania wanavyonituma kuwakalisha muziki wa singeli”.