Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai amefanya mabadiliko ya kamati mbalimbali za kudumu za bunge kwa mujibu wa Ibara ya 96 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania 1977.

Taarifa ya bunge iliyotolewa leo imesema kuwa ibara hiyo ya 96, imelipa uhalali Bunge la Jamuhuri ya Muungano Tanzania kuunda kamati za Bunge za namna mbalimbali kadri itakavyoona inafaa kwa ajili ya utekelezaji bora wa madaraka yake.
Aidha ibara hiyo imeweka wazi kwamba kanuni za kudumu za Bunge zitafafanua muundo wa shughuli za kamati za Bunge.
Kwa msingi huo kanuni ya 118 ya kanuni ya kudumu za Bunge, toleo la Januari 2016 imeweka kamati za kudumu za Bunge zenye muundo wa majukumu mbalimbali kama yanavyofafanuliwa kwenye nyongeza ya nne.
Uteuzi wa waunge kwenye kamati mbalimbali umewekwa utaratibu katika kamati ya 116 . Aidha kanuni ya 116(7) inaweka utaratibu kwamba ,ujumbe kwenye kamati za kudumu za Bunge utadumu mpaka mwisho wa mkutano wa kumi wa Bunge ambao ni nusu ya kwanza ya maisha ya Bunge.
Ikumbukwe kwamba mnamo tarehe 21 Januari 2016 kupitia waraka wa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai namba 02/2016 alifanya uteuzi wa ujumbe katika kamati mbalimbali za Bunge.
Ambapo kamati hizo zimetekeleza majukumu yake mpaka tarehe 9 Februari , 2018 ambapo ni mwisho wa mkutano wa kumi wa Bunge ambao unakamilisha nusu ya uhai wa Bunge la kumi na moja. Hivyo kwa mujibu wa kanuni ya 116(7), kipindi hicho ndio ukomo wa ujumbe katika kamati walizokua wakizifanyia kazi wabunge.
Hivyo kwa mamlaka aliyopewa Spika na kanuni ya 116(3) na kwa kuzingatia vigezo vilivyoainishwa katika kanuni ya 116(5) amefanya uteuzi mpya wa wajumbe katika kamati za kudumu za Bunge na wajumbe wa kila kamati ya kudumu wanawajibika kuchagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti kwa mujibu wa kanuni ya 116(10) kuwa viongozi wao.